aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Wednesday, April 2, 2014

MTOTO WA MIAKA 13 ALIYESUMBULIWA NA MGUU MKUBWA SASA MUNGU AMETENDA

HATIMAYE  Mtoto, Hamisi Hashimu Liguya (13) mkazi wa Yombo jijini Dar amerejea nchini kutoka India alikopelekwa  kwa matibabu akiwa na tabasamu  akiamini kwamba, Mungu amemtendea miujiza, 
Mtoto, Hamisi Hashimu Liguya (13) wakati akiwasili nchini India kwa matibabu.
Hamisi aliyekuwa akisumbuliwa na uvimbe mkubwa wa mguu wa kushoto kiasi cha kushindwa kutembea na kuishia kutambaa amerejea akiwa na matumaini ya kutimiza ndoto zake.
Mtoto huyo alipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Ganga, Tamil Nadu, India ametua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNI) jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita akiambatana na baba yake mzazi, Hashim Liguya.
Daktari wa hospitalia hiyo, Raja Sabapathy kwa niaba ya madaktari wenzake amemwandikia mmoja wa waandishi wetu barua pepe akifurahia kitendo cha Hamisi  kutembea ingawaje kwa msaada wa magongo.
Mtoto Hamisi Hashimu Liguya akiwa na baba yake mzazi hospitalini nchini India.
“Uwezekano wa Hamisi kupona ulikuwa  mdogo, lakini Mungu ametenda miujiza, baada ya kuukata mguu wake na kumtengenezea wa bandia, tulifurahi kuona ameuumudu vyema mguu huo,” aliandika Dk. Sabapathy.
Daktari huyo aliongeza kuwa, Hamisi amekuwa na furaha baada ya kumuondolea uvimbe wa kilo tano  katika mguu wake na kusisitiza kuwa mtoto huyo anahitaji mazoezi ya kila siku ili kuuzoea mguu wake wa bandia.
Hamisi Hashimu Liguya akiwa Hospitali ya Ganga, Tamil Nadu, nchini India kabla ya kukatwa mguu.
Mara baada ya kutua uwanja wa ndege, Hamisi alisema  kuwa ameyafurahia matibabu aliyoyapata India, kwani hakutegemea kama angeweza kwenda na kurudi akiwa anatembea na kuwa na matumaini mapya.
“ Nimefurahi sana, naamini sasa nitaweza kutimiza ndoto zangu kwa kuwa, naweza kutembea,” alisema  Hamisi huku akiwashukuru Watanzania kwa misaada waliyopitia kupitia Global Publishers na Mtangazaji Hoyce Temu.
Mtoto Hamisi akifanya mazoezi.
Baba mzazi wa mtoto huyo alitoa shukrani zake za dhati kwa Watanzania wote waliojitolea kumchangia mtoto wake na kusema kuwa hana cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea dua na kuwataka waendelee na moyo huohuo kwa watu wengine.
“ Furaha yangu imezidi kikomo, sikuwa na matumaini ya kumuona mwanangu akitembea tena, nawashukuru Watanzania kwa wema wao,” alisema baba huyo.
Mtoto Hamisi wakati akipokelewa nchini India.
Watanzania waliitikia wito wa kumchangia fedha Hamisi baada ya kuhamasishwa na Kampuni ya Global Publishers wachapishaji wa Magazeti  Pendwa  Tanzania na Mtangazaji wa Kipindi cha Mimi na Tanzania, Hoyce Temu.
Pia, hamasa nyingine zilitoka kwa Kikundi cha Mkono kwa Mkono ambacho kilionesha jitihada za kumsaidia Hamisi.
Hamisi aliondoka Tanzania, Februari 28, mwaka huu  kwenda  India  kwa ajili ya matibabu hayo akiwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao kitaalam unajulikana kwa jina la plexiform neurofibromatusis.

No comments:

Post a Comment