aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Thursday, December 19, 2013

MTOTO WA MBARAKA MWISHEHE AWASHAMBULIA NA KUWAPIGA VISU WATU WAWILI WA FAMILIA MOJA NUSURA AUE



MASIKU Mbaraka Mwishehe ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Kinondoni, Dar es Salaam kwa madai ya kuwashambulia kwa kisu watu wawili wa familia moja.
Tukio hili lilitokea hivi karibuni Mwananyamala Kisiwani, Dar ambapo kwa mujibu wa taarifa ya kipolisi, mtuhumiwa huyo alikutwa ndani ya nyumba ya Nelson Ainea Shoo, saa kumi na moja alfajiri.
Akizungumza na Amani, mke wa Nelson aliyejitambulisha kwa jina la Neema Hamis Zame (32), alikuwa na haya ya kusema:
“Siku ya tukio, ilikuwa alfajiri kabla hatujaamka, ghafla nilimsikia shemeji yangu aitwaye Goodluck (Ainea Shoo) akipiga kelele na kusema: ‘Kaka kuna mwizi.’ Mume wangu aliamka akatoka kuelekea sebuleni na mimi nilikuwa nyuma yake.

“Kufika, tulimkuta shemeji amelala sakafuni huku utumbo ukiwa nje na damu nyingi zikimtoka, alikuwa akikoroma, kumbe alichomwa kisu kwenye paja, mara mbili tumboni na begani.
“Nilikimbilia chumbani kuchukua khanga na kumfunga ili kuzuia damu isitoke kwa wingi, pia utumbo usiendelee kumwagika huku mume wangu akimdhibiti yule mtu.
“Cha ajabu, muda mfupi mume wangu naye akawa chini anatokwa damu, kumbe hata yeye alikuwa amechomwa kisu mara tatu tumboni na utumbo ukatoka nje.
“Hali ndani ilikuwa mbaya, sakafu ilitapakaa damu. Nikamwita shemeji yangu mwingine aitwaye Erick (Ainea Shoo), yeye akapambana na yule mtu wakati mimi nawahudumia wale majeruhi.

“Nilipata akili za haraka, nilikwenda kumuita mlinzi akaingia na kushirikiana na shemeji wakamdhibiti. Huwezi kuamini, eti yule mtu akaomba asamehewe kwa vile hakujua kama alikuwa ameingia katika nyumba yetu.
“Hakuna aliyemsikiliza kwani alikuwa amefanya kosa kubwa, akaingizwa kwenye gari hadi polisi kuchukua PF3 na likafunguliwa jalada (OB/RB/20201/2013 Kujeruhi) kisha majeruhi tukawapeleka Hospitali ya Muhimbili.
“Kilichotokea hospitali,  shemeji alitolewa bandama kwa vile iliharibika kutokana na majeraha ya kisu,” alisema Neema.
Naye baba mzazi wa majeruhi hao, mzee Ainea Shoo ambaye alitoka Machame Moshi, Kilimanjaro baada ya kupata taarifa hizo, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na dhamira ya kuwatoa roho watoto wake hao, akaliomba jeshi la polisi kushughulikia kesi hiyo kwa uwazi na kuhakikisha haki inatendeka.

Mlinzi wa nyumba hiyo, Boli Mtumwa alipohojiwa na gazeti hili alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema yeye na mdogo wa Nelson ndiyo waliomdhibiti mtuhumiwa na kumpeleka polisi.
Dada wa mtuhumiwa aliyejitambulisha kwa jina la Taji Mbaraka alikiri kukamatwa kwa kaka yake huyo lakini hakuwa tayari kuzungumza zaidi kwa sababu suala hilo lipo mkononi mwa dola.
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, ACP Yusuf Mrefu alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa huku upelelezi ukiendelea.

-GPL


No comments:

Post a Comment