aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Friday, January 31, 2014

Wavaa milegezo na vimini sasa kuanza kuchapwa viboko nchini Tanzania

MKUTANO Mkuu wa Kijiji cha Olgilai wilayani Arumeru umeazimia kuwachapa viboko vijana wa kiume wanaovaa suruali chini ya makalio pamoja na wanawake wanaovaa sketi fupi na suruali zinazobana. Azimio hilo pia limeelekezwa kwa wanafunzi wanaopata mimba au kuozeshwa na kuacha masomo bila sababu za msingi.
 
Mkutano huo umepitisha maazimio saba yanayolenga kurejesha nidhamu na heshima kijijini Olgilai limefikiwa kutokana na vijana wa kike na kiume kuvaa nguo zisizo na heshima.
 
Mwenyekiti wa Kijiji cha Olgilai, Godson Boazi katika barua yake ya Januari 24 mwaka huu kwa viongozi wa makanisa kijijini hapo, aliwaomba kuunga mkono hatua hiyo katika kurekebisha tabia ndani ya jamii yao.
 
“Viongozi wa dini tunafahamu kazi kubwa ya kutunza kundi la Mungu likae kwenye maadili mema. Hivyo basi tunaomba mtusaidie jukumu hili ambalo tumeambatanisha barua kwenu,”alisema Boaz na kuongeza:
“Viongozi wa dini tumewaandikia waraka huu tukijua kwamba ninyi ni watu muhimu katika kusaidia jambo hili na kuwafikishia taarifa waumini wenu wote wakubwa kwa wadogo.”
 
Katika barua yake ambayo MTANZANIA inayo nakala yake Mwenyekiti huyo alisema kwa kauli moja uongozi mkutano huo uliafiki suala hili na kuamuru lianze kutumiwa Januari 24 mwaka huu.
 
Aliyataja maazimio yaliyopitishwa kuwa ni vijana wanaokaa au kusimama ovyo barabarani na maeneo mengine bila shughuli maalumu watachapwa viboko.
 
Jingine ni kuwachapa viboko wote watakaovaa nguo zisizofaa katika jamii yao mfano sketi fupi, suruali zilizobana kwa wasichana na akina mama.
 
“Vijana wa kiume wanaovaa suruali zinazojulikana kama mlegezo, uendeshaji ovyo wa pikipiki, wavutaji wa bangi, dawa za kulevya, gongo na wanywaji wa viroba, uchezaji kamari na karata.
 
“Wanaotukana ovyo barabarani na kupiga kelele za uvunjaji wa amani, wezi wa vitu vikubwa na vidogo kama kuku, ndizi, viazi, mahindi na mboga shambani watashughulikiwa,” alisema Boazi.
 
Alisema Mkutano Mkuu wa Kijiji ulijiridhisha kuwa matendo hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa nidhamu kijijini hapo na maeneo mengine.