aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Sunday, January 19, 2014

Wananchi Kiteto wamshangaa Pinda

PindaWANANCHI wa Wilaya ya Kiteto wamemshangaa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na ziara yake aliyoifanya juzi na kujionea athari zilizotokana na mapigano ya wakulima na wafugaji. Wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana wilayani hapa kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema ziara ya Pinda haikuwa na manufaa yoyote kwao, kutokana na kiongozi huyo kukataa kuwasikiliza.
Hata hivyo, wananchi hao walisema ziara ya Pinda wilayani hapa haina tija, kwani ameshindwa kuchukua hatua dhidi ya viongozi waliohusika katika kuchochea na kupalilia mgogoro huo.
Mfugaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kisioki Mesiaya, alisema kitendo cha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi bila kuruhusu maswali kimeashiria viongozi kulindana wanapokosea.
Alisema lengo la Pinda kuja Kiteto lilikuwa ni kuzungumza na wananchi, kisha atoe tamko la Serikali kuhusu maafa ya kinyama yaliyotokea kati ya wakulima na wafugaji, lakini hakufanya hivyo.
“Sikutegemea Waziri Mkuu kama angekataa kuulizwa maswali na wananchi, sioni kuwa hapa amefuata nini, kama ilikuwa hoja ni kutoa tamko angeweza kutolea Dar es Salaam si Kiteto,” alisema.
Mfugaji mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema: “Wafugaji tulichangishwa mamilioni ya fedha, Waziri Mkuu alikiri kuwa tumechangishwa na viongozi wa halmashauri.
“Iweje leo tunaambiwa tutoke wote kwenye hifadhi, nani ataturejeshea fedha zetu? Tunataka turejeshewe madume yetu ya ng’ombe, hatukubali,” alisema mwananchi huyo.
Kwa upande wake, Mwajuma Sendaro (mkulima) alishangazwa na kauli ya Waziri Mkuu ya kutaka watu waliopo katika eneo hilo waondoke, kwamba haijazingatia msingi wa tatizo.
“Mfugaji ataondoka na mifugo yake katika eneo la Emboley Murtangos, ambalo lilimsaidia kuendesha maisha yake, je, mkulima aliyekuwa anategemea shamba lake kuendesha maisha yake ataondoka na nini?
“Hapa hakuna jibu lililotolewa na Serikali kuhusu mauaji na naamini mauaji yataendelea kujitokeza, kwa kuwa hakuna kauli ya Serikali iliyotolewa makini kukemea ama kuzuia maafa yasitokee tena, badala yake Pinda ameacha mianya ya kuendelea kujitokeza maafa zaidi,” alisema Sendaro.
Mwananchi huyo alisema Waziri Mkuu alitoa kauli zenye utata ambazo hadi sasa wananchi wameshindwa kuelewa.
“Huwezi kutoa kauli mbili kuhusu jambo moja, huku akisema watu waliopo katika eneo hilo waondoke, na nyingine Serikali iwalinde wale wote waliopo katika eneo hilo, wakati ufumbuzi unatafutwa na Serikali, sasa tutafuata lipi?” alihoji.
Naye Salum Rashidi (mkulima) alisema alitarajia kuona hatua kali zinachukuliwa dhidi ya viongozi waliohusika katika mgogoro huo, lakini Pinda ameshindwa kuchukua hatua.
Mkulima mwingine, Selemani Mtae alisema: “Waziri Mkuu amewatega wananchi wa Kiteto, taarifa yote anayo kuhusu mgogoro huu, kazi yake ilikuwa ni kuchukua hatua kukomesha hali hii, lakini yeye amefanya siasa”.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana, Isaya Chambala, alisema matokeo ya mauaji hayo yanatokana na uzembe wa wazi wa kutochukuliwa hatua mapema na viongozi wa Wilaya na Mkoa, baada ya kulalamikiwa kwa muda mrefu.
Alisema migogoro ya ardhi wilayani Kiteto ni ya muda mrefu, lakini kutokana na baadhi ya viongozi kuendekeza rushwa, siasa, ukabila, ndio uliofikisha mgogoro huo hapo ulipo.
Awali akizungumza na mamia ya wananchi wilayani humo akiwa katika uwanja wa Shule ya Msingi Kibaya, Pinda alisema baada ya kutembelea eneo linalogombaniwa na wakulima na wafugaji, alichokuta ni mashamba ya wakulima na si hifadhi.
“Kabla ya kuzungumza nanyi, nikasema hebu niende kuona eneo hilo la Hifadhi ya Emboley Murtangos kwa kutumia helikopta, hapo aah…haifananii kuwa hifadhi, bali nilichokiona ni mashamba ya wakulima,” alisema Pinda.
Pinda alisema upo utata mkubwa aliouona baada ya kusomewa taarifa juu ya uanzishwaji wa hifadhi hiyo, akisema njia pekee ya kutatua mgogoro huo ni kujiridhisha kwa vijiji saba vilivyounda hifadhi hiyo, iwapo jamii ilishirikishwa.
Hata hivyo, Pinda alikwenda mbali na kuagiza uongozi wa Wilaya ya Kiteto na Mkoa wa Manyara kutafuta mihutasari ya vijiji vilivyounda hifadhi hiyo kati ya wakulima na wafugaji, kama wote walishiriki kuunda hifadhi hiyo ya Emboley Murtangos.
Kuhusu suala la halmashauri kuchangisha fedha wafugaji kuwatoa wakulima katika eneo hilo, alisema uongozi wa Wilaya na Mkoa umekosea na kuonya vikali kuwa tabia hizo ni mbaya na hazipaswi kurudiwa.