aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Thursday, January 23, 2014

Unyama! Kigogo wa CCM Mkoani Mbeya Amuunguza Yatima kwa maji ya Moto Kifuani kwa kosa la Ulafi..!

SIKU zote tumezoea kuona baadhi yawanasiasa na viongozi wakiwa mstari wa mbele kupinga ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na hata kupinga ajira kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Hali hiyo imekuwa ni tofauti kwa Kigogo mmoja wa Chama Tawala CCM wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambaye mbali na kumtumikisha mtoto aliyechini ya miaka 18 bali pia amemfanyia unyama na ukatili uliopitiliza kwa kummwagia maji ya moto kwa kile kinachodaiwa kuwa mtoto huyo anakula sana.
Kigogo huyo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Kitongoji cha Mahango kijiji cha Mageya kata ya Rujewa wilayani Mbarali aliyefahamika kwa jina la Ziada Bakari Mwihesi anadaiwa kummwagia maji ya moto mtoto Agustino Sanga(12) ambaye alikuwa akimtumikisha kwa kufanya kazi za  kuchunga mifugo yake kuanzia alfajiri hadi usiku bila kumpatia chakula cha uhakika.
Mtoto Agustino ambaye ni yatima anayelelewa na bibi yake baada ya kufiwa na wazazi wake huko wilayani Makete mkoani Njombe alianza kuishi na Mwenyekiti huyo wa chama mwaka 2011 akitokea wilayani Makete mkoani Njombe ambapo Bibi yake kutokana na kutokuwa na uwezo alimkabidhi mama huyo ili aishi naye huku akimsaidia kazi za kuchunga mifugo yake.
 jamani
Akizungumza mkasa huo mbele ya mwandishi wa habari hizi aliyefika kijijini hapo  kufuatilia taarifa za unyanyasaji dhidi yake, mtoto huyo alisema kuwa aliletwa nyumbani kwa mama huyo mwaka 2011 na Bibi yake akitokea Wilayani Makete Mkoani Njombe ili aweze kufanya kazi ya kuchunga ng’ombe kwa mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa tukio la kuunguzwa moto lilimtokea mwezi Juni 2013 shambani kwa Mwenyekiti huyo eneo la Jangulutu majira ya usiku ambapo Mwenyekiti huyo alianza kumsimanga kwa madai kuwa amekuwa akila chakula kupita kiasi na  kusababisha watoto wake kutoshiba.
Mtoto Agustino aliendelea kusema kuwa, mama huyo aliendelea kumsimanga na ghafla alichukua maji yaliyoinjikwa jikoni yakiwa yamechemka kwa ajili ya kupika ubwabwa  usiku huo na kummwagia kifuani na baadaye kumfungia ndani huku akilia kwa uchungu.
“Nilipata uchungu mkubwa, nililia sana sikuwa na msaada wowote usiku ule mama Yule alinifungia ndani, sikupata matibabu yoyote,’’aliongea kwa uchungu mtoto Agustino.
Agustino aliendelea kufafanua mkasa huo kwa kusema kuwa  akiwa amefungiwa ndani mama huyo alikuwa akisaga  mifupa ya ng’ombe na kumpaka katika jeraha la kidonda alichounguzwa na kwamba kila alipokuwa akimpaka ndipo kidonda kilipozidi kutoa usaha.
Alisema akiwa ndani Bibi yake alianza kumtafuta ndipo siku hiyo alipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumuuliza alipo ambapo alimweleza kuwa mjukuu wake aliungua moto alipokuwa akicheza karibu na moto.
Agustino aliendelea kubainisha kuwa tangu alipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo mwaka 2011 hajawahi kupumzika na kwamba amekuwa akitumikishwa kama Punda kuanzia alfajiri hadi usiku huku akipewa chakula kidogo.
Kwa upande wake Babu wa Mtoto huyo Method Ndelwa(55) Mkazi wa Kitongoji cha Mahango alisema mtoto huyo baada ya kufika nyumbani hapo alikuja mume wa Mwenyekiti aitwaye Seleleka Twasanga na kumuomba mtoto huyo awe anamchungia ng’ombe na mbuzi shambani kwake.
Alisema tangu mjukuu wake  alipoungua mwaka 2013 mwezi wa 6  hakuna msaada wowote ambao unatolewa na familia ya Mwenyekiti na kwamba ameendelea kuugulia na majereha yake bila kupatiwa matibabu ya uhakika.
“Mimi na Bibi wa wa mtoto huyu hatuna hali zetu ni duni  kipato chetu ni kidogo kama mnavyoona kidonda cha mtoto kinatoa usaha na hapo mwanzo kilikuwa kinatoa funza, mama mmoja Rukia Shomari alitusaidia kumnunulia dawa,’’alisema Babu wa mtoto huyo.
Alisema kuwa hakuwa anajua utaratibu wowote wa kutoa taarifa hizo kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Polisi na kwamba tangu alipounguzwa moto walikuwa wakimuangalia tu mtoto huyo huku wakishindwa kujua  hatima yake.
“Tunaomba mtusaidie kulifikisha hili ili jamii ijue kama mna uwezo wa kumsaidia mtoto huyu tunaomba msaada wenu kumuokoa mtoto huyu’’,alisema Mzee Ndelwa.
kigogo2
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahango ambaye ndiye anayedaiwa kufanya unyama huo,Ziada Mwihesi alikana kumchoma moto mtoto huyo na kudai kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na mume wake aliyemtambulisha kwa jina la Seleleka kuwa mtoto Agustino ameungua moto  ndipo alipoondoka na kwenda shambani na kumkuta mtoto huyo akiwa ameungua kifuani.
Hata hivyo  Mwenyekiti huyo anadai kuwa  chanzo cha mtoto huyo kuungua ni kutokana na kuota moto asubuhi  wakati akipasha kiporo cha wali katika jiko la kuni na kusema kuwa mtoto huyo alishaungua moto akiwa  kwa bibi yake na kudai kuwa hapo amekuja kuungua kwa mara ya pili.
Pamoja na kufanya unyama huo Mwenyekiti huyo alionekana kutohitaji kutoa ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi kwa kutoa majibu ya mkato wakati alipokuwa akiendelea kuulizwa maswali  juu ya kuchomwa moto kwa mtoto huyo ambapo pia alikanusha kummwagia maji ya moto mtoto huyo kwa madai ya kumaliza chakula.
Naye  Mume wa Mama huyo Seleleka Twasanga alikiri kuungua kwa mtoto huyo na kudai kuwa yeye alipata taarifa baada ya kupigiwa simu na jirani yake ambaye wapo jirani shambani  kwamba Mtoto Agustino ameungua moto ndipo alipoondoka na kwenda shambani ili kujua chanzo cha tukio hilo.
Bw.Twasanga alisema wakati anamchukua mtoto huyo kwa Bibi yake walifanya kama kubadilishana na Bibi huyo ambaye alihitaji kila mwaka alimiwe shamba la heka mbili kwa ng’ombe wakati mtoto Agustino akifanya kazi ya kulima na kuchunga Ng’ombe na mbuzi shambani kwa Twasanga.
Akielezea zaidi mume wa mama huyo alisema aliendelea kumlimia shamba bibi wa mtoto Agustino na kukiri kutomlipa chochote zaidi ya bibi huyo kulimiwa shamba.
Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kimekuwa katika harakati za kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo unyanyasaji wa wanawake na Watoto.
Mkurugenzi wa TAMWA Valerie Msokwa kupitia jarida lake linalotolewa na taasisi hiyo alisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria ya Kimataifa ya haki ya mtoto ya mwaka 2009 iliyowekwa katika tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Mtoto linalotoa mwongozo wa kulinda na kutambua haki za mtoto nchini.
Alisema watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa watoto katika maeneo mengi ya mijini na vijijini.
Naye Diwani wa Kata y Rujewa Bi.Gurzar Sabil alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo la kinyama la mwenyekiti huyo alisema kuwa  hana taarifa hiyo lakini aliahidi kuwasiliana na Ofisa Ustawi wa jamii wilaya ya Mbarali ili waweze kwenda nyumbani kwa mtoto waweze kumsaidia ikiwa ni pamoja na kumkamata mtuhumiwa.
kigogo3
Mara baada ya Mwandishi wa habari hizii kuondoka wilayani humo Ofisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Mbarali Winifrida Mahali akiambatana na Mratibu wa Dawati la Jinsia wilayani humo Christa Komba walifika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumchukua hadi kituo cha Polisi.
Bi Mahali alisema kuwa walimfuata mtuhumiwa pamoja na mumewe na kuwapeleka kituo cha polisi ambako walilala hadi asubuhi  na kufikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbarali ambako wamesomewa mashtaka ya kujeruhi na wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana hadi Januari 29.

No comments:

Post a Comment