MWANAMKE mmoja amekamatwa na raia wema katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara, na kupelekwa polisi baada ya kunyanyasa mtoto wa kambo wa miaka minne, kwa kumpiga na kumlisha kinyesi chake kwa madai kuwa amejisaidia ndani ya nyumba yake.
Mwanamke huyo, Joyce Maneno, mkazi wa Mtaa wa Idara ya Maji katika mji wa Bunda, amekamatwa na wananchi wa eneo hilo, baada ya kugundua kunyanyaswa kwa mtoto huyo, kwa kumchapa, kumpiga, na kumlisha kinyesi chake.
“Sisi tuligundua baada ya kila siku kusikia mtoto analia kwa kipigo, tena alikuwa akimpiga kwa kumtoa nje, eti kosa amejisaidia haja kubwa ndani ya nyumba yao na pia fimbo aliyompigia ndio aliyokuwa akichovya kinyesi na kumlisha…,” alisema mwanamke mmoja mkazi wa eneo hilo.
Wakitoa maelezo na kuthibitibishwa na maofisa wa jeshi la polisi wilayani hapa, wananchi hao walisema mwanamke huyo amekuwa akifanya ukatili huo mara kwa mara, na kwamba anafanya hivyo wakati mume wake amekwenda visiwani kwenye shughuli zake za uvuvi.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bunda, Chiku Mshora, amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa baada ya mwanamke huyo kudhaminiwa polisi, alisikika akijigamba kuwa mtoto huyo atamfanyia jambo lolote lile, kwani hawezi kumharibia maisha yake kwa mumewe.
Wakati huo huo, mtoto mwenye umri wa miaka 12 aliyekuwa ameozwa kwa mwanaume wa miaka 54, amepelekwa kwenye kituo cha kulea watoto kiitwacho Jipe Moyo, kilichoko mjini Musoma, ili aweze kutunzwa huko na kusomeshwa.
Mtoto huyo alikuwa ameolewa na mzee huyo, baada ya kutoa kishika uchumba kiasi cha Sh 55,000 kwa baba yake mzazi, ambapo sasa mzee huyo pamoja na baba, wako mahabusu baada ya kunyimwa dhamana na mahakama ya wilaya ya Bunda, kwa kushindwa masharti ya dhamana.
No comments:
Post a Comment