INAWEZA kukushtua lakini ndivyo ilivyotokea. Kichanga cha siku thelathini, Veis Venus kiliibwa hivi karibuni, mtuhumiwa akiwa ni mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Grace akidaiwa ni mjamzito feki.
Tukio hilo la kushangaza lilijiri Januari 27, 2013 maeneo ya Posta jijini Dar na mtoto huyo kupatikana Januari mwaka huu, mkoani Mbeya.
Akizungumza na waandishi wetu juzi nyumbani kwake, Kawe ya Tanganyika Parkers, Dar, mama mzazi wa mtoto huyo, Salma alisimulia kisa kizima:
“Ilikuwa Januari 24, mwaka jana, marafiki zangu watatu walikutana na mwanamke aliyesema ana taasisi inayotoa misaada kwa watoto.
“Kwa sababu nilihitaji, nikambeba mwanangu na kwenda Mwenge ambako nilionana na mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Grace.
“Aliniambia asingetoa msaada mpaka Sikukuu ya Krismasi na Boxing Day zipite. Januari 27 nikakutane naye.
”Cha kushangaza siku hiyo sikumkuta Grace bali mwingine aitwaye Suzana. Alisema ni mfanyakazi wa Grace.
“Siku hiyo nilikuwa na mwanamke mwingine naye ana mtoto. Suzana akatuambia wana ofisi Mlimani City na Posta, hivyo tulitakiwa kwenda Posta kupokea misaada hiyo.
“Kufika kituoni, Suzana akashauri mimi na mwenzangu tupande daladala, yeye na watoto wetu wapande Bajaj tukakutane Posta.
“Dakika chache mbele akabadili kauli, akasema yeye aondoke na mtoto mmoja tu na alimchagua mwanangu.
“Tulipanda daladala mpaka Posta ambapo tuliwasiliana na Suzana akasema yupo kwenye foleni. Tulimsubiri kwa muda, tulipompigia tena simu yake ikawa haipatikani.
“Ilibidi tumpigie simu Grace, akasema Suzana alipitia Kigamboni kuchukua misaada hivyo tumsubiri. Tuliendelea kusubiri hadi saa kumi na mbili jioni, hakuna aliyekuwa akipatikana kwenye simu,” alisema Salma.
Salma: Nililia sana jamani! Nilisema moyoni sitaki tena msaada namtaka mtoto wangu lakini hakuwepo. Niliwapa habari ndugu kisha tukaenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kawe na Kituo cha Polisi Sitakishari jijini Dar kwa vile mtu wa kwanza kuniambia habari za msaada anaishi huko.
Naye shangazi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Selina alikuwa na haya ya kusema:
“Baada ya kupokea habari kutoka kwa Salma tulichukua namba za wale wezi na kwenda nazo kampuni moja ya simu kuziangalia.
“Desemba 30, mtu wa kampuni hiyo aliwaambia polisi, Suzana yupo Mbeya. Januari 18, bila kutarajia, Grace na Suzana wakatiwa mbaroni huko Mbeya. Grace alidai eti mtoto ni wake.
“Januari 19, polisi waliwachukua wote na kurudi nao Dar kwa ajili ya vipimo vya DNA vya Grace, Salma na mtoto Veis.
“Baada ya vipimo, majibu yalionesha mtoto ni wa Salma huku Grace na Suzana wakiwekwa chini ya ulinzi wa polisi na kufanya taratibu za kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema Selina.
Habari za kipolisi zinadai kuwa, Grace alipobanwa zaidi alisema alimwiba mtoto huyo kwa vile hakuwahi kuzaa na kwamba alimdanganya mumewe (hakumtaja jina) anayeishi Rukwa kwamba ana mimba hivyo alikuwa Mbeya kujifungua.
No comments:
Post a Comment