aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Wednesday, August 21, 2013

UTATA MTUPU FILAMU YA SHEIKH PONDA NA WENZAKE...

 
IMENIBIDI niandike, ingawa sikupenda kufanya hivyo katika sakata la Sheikh Issa Ponda na wenzake. Naandika ili kuweka kumbukumbu sawa, wenye maswali kama ya kwangu wajue kwamba si wao tu, bali tuko wengi tunaowaza na kuona mambo kama wao.

Sikupenda kutumia ufahamu, maarifa na ujuzi wangu kuiandika filamu PondSikupenda kutumia ufahamu, maarifa na ujuzi wangu kuiandika filamu Ponda na wenzake, inayooneka kuacha maswali mengi kuliko majibu. Tena maswali yasiyokuwa na manufaa au maslahi mapana kwa jamii na kwa taifa. Pia, ningependa ieleweke mapema kwamba ninayaandika haya, nikiwa najilazimisha kwa sababu si vizuri kuacha kumbukumbu za maswali na mtazamo mbaya katika jamii.

Kutokana na maswali kuwa mengi kuliko majibu, ndiyo sababu wakati filamu ya sheikh Ponda na wenzake inaendelea, ilinibidi kugonga hodi kwa msajili wa “dini na vyama vya hiari”, iliyopo katika Wizara ya Mambo ya Ndani. Lengo la kwenda kwa msajili ni kutafuta na kupata jibu la swali, kinachoitwa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, ni nini na kilisajiliwa lini na kwa malengo gani na ofisi zao ziko wapi?
Safari yangu hiyo, haikuzaa matunda kwa sababu msajili wa dini na NGO’s sikumwona. Hakuwepo ofisini na kama ilivyozoeleka katika ofisi za umma zilizo nyingi, kila mtu hataki kusema akidai si msemaji na pengine hata wasemaji hawasemi. Baada ya jibu hilo, nilisimama nje ya ofisi hiyo nikiwa nimechoka, maana raha ya mtafutaji ni kupata anachokitafuta.
Nikiwa bado nimesimama, nikasikia madereva wa magari ya viongozi wa wizara hiyo wakipiga soga, lakini mjadala ukiwa ni mwendelezo wa ‘filamu ya Ponda na wenzake’. Mjadala unanivuta kuwasogelea na kujumuika nao, maana waswahili tunao msemo usemao:- “Sikio halilali njaa..!”.
Kadri mjadala unavyokolea, ndiyo ninavyogundua kwamba madereva hao wanayo majibu ya maswali magumu yaliyonifanya nifunge safari ya kwenda hapo wizarani ingawa taarifa zao si rasmi. Dereva mmoja anasema:- “Kama kuna siku nitakutana na Sheikh Ponda Issa Ponda, nitamuuliza maswali. Aniambie, kwa nini anatumia taasisi hewa (isiyosajiliwa na kutambulika kwa mujibu wa sheria za nchi) kuuchafua uislamu?”
Jamaa (dereva) anaendelea kusema, “ukweli hivi sasa dini yetu (ya kiislamu) imechafuka sana. Kundi la hawa jamaa limetuchafua sana katika jamii, kiasi kwamba ninaamini kila mtu anajua waislamu tuna fujo na vurugu, mimi jambo hilo linaniuma sana. Uislamu ni dini ya amani na kwa zama hizi, uwezi kueneza dini kwa harakati za mapambano ya kimabavu”.
Msomaji, mjadala huo wa madereva wa viongozi wa wizara ya mambo ya ndani unaakisi hali ya mambo katika jamii. Kwamba miongoni mwa jamii, wapo waliokinai na wanaokerwa tena wako tayari kufanya mambo kwa namna ambayo haitarajiwi ili kuhakikisha heshima, hadhi na haiba ya dini yao (ya kiislamu) haichafuliwi na watu wachache. Hawa wanaamini kwamba, harakati za kueneza dini yao (ya kiislamu), inatatizwa na makundi yanayotaka kueneza dini hiyo kwa fujo na vurugu.
Nikirejea maelezo ya madereva wale kwamba kinachoitwa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, ni taasisi hewa. Je imekuwaje taasisi hiyo imekuwa ikiwasiliana na serikali kwa nembo hiyo? Je, siku hizi serikali inafanya kazi kwa namna gani au inapenda jamii iendelee kuamini kwamba hiyo pia ni moja ya taasisi zilizoanzishwa na wana usalama, ili kupitisha ajenda zao wanapohitaji kufanya hivyo?
Itakumbukwa kwamba, viongozi wa taasisi hiyo hewa walialikwa katika semina kuhusu sensa na mwisho wake kukaibuka harakati za kuipinga sensa. Pia, hivi karibuni taasisi hiyo imemwandikia waziri mkuu kupinga mpango wa kuanzisha kamati za ulinzi na usalama katika msikiti. Je, wangewezaje kumuandikia kama si taasisi inayotambulika na kukubalika kwa viongozi wakubwa serikalini?
Wiki iliyopita, gazeti moja lilinukuu chanzo chake cha habari likisema:- ”Hapo utashangaa watu hao walifikiria nini, kwa sababu waliitwa katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, chini ya Mkuu wa Mkoa huo wa Morogoro, ….kisha wakaelezwa mapema kabisa kuwa Ponda akionekana, polisi watamkamata! Lakini bado wakakaidi na kukiuka makubaliano yale ya kistaarabu kabisa”.
Swali ambalo bado najiuliza ni hili, ilikuwaje kamati ya ulinzi na usalama iwe ni mtoa siri kwamba akitokea Ponda, polisi watamkamata? Je, walitaka aendelee kuwa mafichoni na polisi washindwe kumnasa na kumfikisha mahakamani kwa tuhuma zinazomkabili?
Maswali mengine yanayochanganya katika filamu hii ni kwamba, katika maeneo ya ibada kama hilo, wafuasi au waamini kwa kawaida huwa ni watii na waaminifu kwa kiongozi wao wa kiroho. Je, wanapoamua kurusha mawe dhidi ya polisi, wanafanya hivyo bila ruhusa ya viongozi wao, au walilazimika kumtii mmoja wa viongozi wao, naye ni nani maana kama yupo naye alitenda kosa kwa kuhamasisha au kuagiza watu kuwazuia polisi kufanya kazi yao.
Wengine wanajiuliza na kujadiliana wakisema:- Sheikh Ponda anaendelea kutumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja, kifungo hicho bado hakijakwisha, kinaambatana na masharti kwamba asitende kosa lolote katika kipindi hicho. Lakini katika hali ya uungwana wa kawaida, kwa mtu aliye katika uangalizi huo wa kisheria, anapotuhumiwa kufanya kosa na kutangazwa katika vyombo vya habari kwamba anatakiwa kukamatwa au ajisalimishe, kwa nini ukatae kujisalimisha au awakimbie polisi mpaka yamkute haya? 
Kwa muungwana tena ambaye anatajwa kuwa ni kiongozi, anapaswa kuonesha mfano bora kwa umma anaouongoza katika kuzitii mamlaka halali na tena kutii sheria bila shuruti. Ndiyo sababu kwa kuyasoma mazingira yote ya filamu ya Ponda na wenzake, kunatoa viashiria kwamba Watanzania wanatakiwa kuelimishwa ili kuyatambua matakwa ya kisheria, ili kuepuka matendo yanayoweza kutafsiriwa kwamba ni kuvizuia vyombo vya dola kulinda, kuhoji au kukamata kwamba ni kuvizuia vyombo hivyo kufanya kazi yao jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi. 
Pamoja na hayo watu wanauliza kuwa, baada ya kiongozi huyo kujeruhiwa na kupelekwa hospitali na kisha kuzuka tafrani baina ya wafuasi wa Ponda na wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, mbona hao waliopigwa na kujeruhiwa wakiwa kazini (hospitalini) na wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Ponda, hakuna anayewasemea ingawa taarifa zipo?
Umma unapenda kufahamu kuwa, baada ya kutoroshwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, kiongozi huyu wa kiroho alipelekwa wapi na kwa nini alipelekwa huko? Je, kulikuwa na wataalamu wa kutosha kumsaidia vema au alipelekwa kufanyiwa majaribio ya kutibu? Akiwa huko je, alifuata taratibu halisi za matibabu yanayotokana na matukio ya namna hiyo, ikiwamo kuwa na fomu ya polisi iitwayo PF3 au alitibiwa kinyemela?
Je, huko alikopelekwa awali kutibiwa, kama hakujulikani vizuri hususan uwezo wa wataalamu na nia iliyokuwapo, kusingekuwa na uwezekano wa kuwapo wasiomtakia mema Ponda na hivyo badala ya kumsaidia, wao wakazidi kumdhuru maana msafara wa mamba siku zote haukosi kenge? Au, basi hakukuwa na uwezekano wa wengine kutaka kupotosha ukweli wa mazingira ya tukio, ili kuwatwika mzigo wale waliotimiza wajibu wao uliolenga kuhakikisha matakwa ya kisheria yanatimizwa dhidi ya Ponda? 
Pia, tunapaswa kujiuliza kwamba tunauhakika gani matibabu aliyoyapata awali akiwa mafichoni yalikuwa ni salama na hakuwekewa kemikali za madhara katika dawa na vifaa vilivyotumika?
Kama wanavyosema wengi, hapa ni pagumu kujua ukweli na kupata majibu ya maswali mengi yanayoibuka. Hivi ni kwa nini alitolewa tena kwa namna ya kibabe katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Morogoro na kufichwa kusikojulikana?
Ni muhimu jamii ikatafakari pia kwamba wakati mwingine hata nje ya siasa, watu wana mbinu kama za wanasiasa wanapotafuta huruma za watu au umaarufu. Sio siri kwa mazingira tuliyomo, busara za Watanzania zinahitajika zaidi kuliko kuongozwa kwa hisia na jazba. 
Hakuna anayefurahia Sheikh Ponda kujeruhiwa, maana ana haki ya kuwa salama na hakuna anayependa kumuona kila wakati anakuwa katika misukosuko na migogoro hata kama pengine yeye ndiye anayeitaka. Lakini pia hakuna anayefurahia kusikia kwamba licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumkuta na hatia na kumpa adhabu ya kifungo cha nje, kwa sharti la kutotenda kosa jingine, eti bado anatuhumiwa kukaidi amri hiyo. Sambamba na hilo ni muhimu wanaoshabikia filamu ya Ponda na wenzake wakafahamu kwamba, sasa Watanzania walio wengi wameanza kuikinai!


Source:Raia Mwema

No comments:

Post a Comment