Jomo Kenyatta.
Ndugu msomaji, kabla sijaelezea nilichokusudia kuzungumza nanyi kupitia safu hii, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuiona siku ya leo nikiwa na afya njema.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Nasema hivyo kwa sababu kuna wenzetu wanakabiliwa na dhiki na magonjwa na wengine licha ya kutegemea kuiona leo, wameshindwa baada ya kukumbwa na mauti. Kwa kuwa mimi na wewe tumejaliwa kuwa wazima, hatunabudi kumshukuru Mungu kwa upendo wake kwetu.Baada ya kusema hayo, sasa ngoja nirejee kwenye jambo ambalo nimeguswa kuliongelea wiki hii lihusulo Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndugu msomaji, Tanzania na Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri kwa muda mrefu, lakini uhusiano huu umeanza kuingia dosari pale rais wetu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alipotoa ushauri kuhusiana na mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kikundi cha waasi cha M23.
Kikwete alikitaka kikundi hicho kiondoke katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati na kumshauri Rais wa Rwanda, Paul Kagame kukaa na wapinzani wao mezani ili kumaliza tatizo.
Kinachonishangaza ni kwamba Rais Kagame amekuwa mbogo baada ya kushauriwa huku majirani wote wa DRC hasa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakiwa wanajua kinachoendelea katika nchi hiyo lakini kila mmoja ameamua kukaa kimya.
Viongozi hao hawajatoa kauli yoyote kwa Rwanda wala huko kwenye vita ambako watu wanauawa hovyo na wengine kubaki na vilema vya maisha.
Rais Kikwete hakukaa kimya baada ya kuona hakuna ufumbuzi wa amani DRC, aliamua kutoa kauli ya upatanishi lakini badala yake ikazua chuki baina yake na Rais Kagame.
Mimi naamini Kagame amekuwa na kisirani dhidi ya Kikwete pale Tanzania ilipoamua kupeleka majeshi yake ndani ya DRC kwa mapendekezo ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa ajili ya kulinda amani huku wakitumia kifungu cha saba cha ulinzi wa ambani wa umoja huo, kinachoruhusu kujibu mashambulizi pale askari wa kulinda amani wanaposhambuliwa.
Hiki ndicho chanzo cha Rais Kagame kuanza kutoa matamshi ya kejeli bila kujielewa dhidi ya Tanzania na rais wake.
Kuna madai kwamba kikundi cha waasi cha M23 kimekuwa kikipora madini nchini DRC na kuyapeleka Rwanda kuyauza. Kama madai hayo ni kweli, basi ni wazi kuwa M23 inasaidia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Rwanda kukua kwa haraka.
Hata hivyo, kama chokochoko hizo na lawama ni kwa ajili ya jeshi la Tanzania kuwa DRC mbona majeshi yanayolinda amani huko kwa Wakongo ni pamoja na yale ya kutoka Afrika Kusini, Msumbiji na Malawi? Kumchachafya Kikwete na Tanzania si ni kutuonea bure?
Wachunguzi wote wa amani wanaona kuwa Rais Kagame amecharuka kwa kuona kuwa ushauri anaopewa akiukubali utafanya waasi wa Kongo kushindwa kwenda nchini kwake kuuza madini wanayopata kwa Kabila hivyo akaona njia pekee aliyoiona inafaa ni kupambana na Rais Kikwete bila kujali kuwa mtazamo wa JK ulikuwa ni kuwasaidia wananchi wa Congo, ambao wanateseka kwa muda mrefu kwa kushambuliwa na majeshi ya M23 na kuuawa, huku wanawake na watoto wakiwa waathirika wakubwa.
Tukirudisha fikra nyuma kabisa tunakumbuka kuwa kilichomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa DR Congo, Dikteta Mobutu Seseseko Kuku Wa Zabanga, ni kikundi cha Banyamulenge kilichofadhiliwa na nchi za Uganda pamoja na Hayati Laurent Kabila, baba yake Rais wa sasa wa Congo, Joseph Kabila.
Hayati Kabila alikaa kwa muda mfupi sana madarakani na yakajitokeza matatizo kati yake na washirika wake Banyamulenge (Rwanda/Uganda), na mara zikaanza vurugu na hatimaye vita rasmi na kusababisha mashambulizi Goma kuelekea Kinshasa hadi Kabila alipoomba msaada kutoka Zimbabwe na Angola.
Majeshi ya nchi hizo za Angola na Zimbabwe yalifanikiwa kuyarudisha nyuma majeshi ya Rwanda na Uganda ingawa baadaye waasi walifanikiwa kujipenyeza na kumuua Rais Kabila lakini walishindwa kumweka kibaraka wao kama walivyokusudia badala yake nafasi yake ikachukuliwa na mwanaye Joseph Kabila ambaye naye amekuwa na misimamo isiyoyumbishwa hadi leo.
Tanzania tuna historia katika Bara la Afrika tangu enzi za Rais wa Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba ilikuwa inasaidia bara hili na watu wake kupata uhuru na amani na ndicho alichoonekana kukifanya Rais Kikwete kwa DRC na nchi zinazoizunguka.
Nilitegemea nchi nyingine za Afrika Mashariki zikiongozwa na Kenya iliyoasisiwa na mzee Jomo Kenyatta zingekaa na kuikemea Rwanda na rais wao Kagame kwamba si vyema kutukana na kukashifu viongozi wenzake ambao wametoa ushauri wa kudumisha amani katika sehemu hii ya Bara la Afrika.
Hakuna amani inayopatikana kwa njia ya vita, hivyo ni vyema akakubali ushauri, umwamba hausaidii katika kuleta amani sehemu yoyote duniani.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment