IBRAHIM Moses, mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam amenaswa na Polisi wa Kituo cha Mwenge kwa madai ya kujifanya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwenye cheo cha kanali.
Kanali feki wa JWTZ, Ibrahim Moses baada ya kunaswa na polisi.
Habari za kipolisi zinadai kuwa Ibra alikuwa akifika Kituo cha Polisi Mwenge mara kwa mara na alikuwa akipewa heshima zote kama afisa wa jeshi na hasa kwa kuwa alikuwa akitoa ushirikiano wakati wa kunasa wahalifu.
...Akiwa mikononi mwa polisi.
“Ilikuwa akikuta watu wamejazana hapa kituoni alikuwa anakuwa mkali na kuhimiza washughulikiwe haraka kwani hapendi kuona watu wamejaa kwenye kituo,” kilisema chanzo chetu kituoni hapo.
...Akipelekwa kituoni.
Habari zinasema baada ya hapo mkuu wa kituo hicho cha polisi ilibidi afanye kazi ya ziada kuwasiliana na wanajeshi wa Kambi ya Lugalo ili kujua kama wana afisa wao anayeitwa Kanali Ibrahimu Moses wa Kitengo cha Usalama wa Taifa na Mawasiliano, wakajibu hawakuwa na askari mwenye jina hilo ndipo ulipoandaliwa mtego wa kumnasa.
Imeelezwa kuwa aliitwa kituoni hapo kwa njia ya simu na kuambiwa kulikuwa na kazi ya kiintelejensia na baada ya saa tatu akawa amewasili na kukamatwa kisha kufungwa pingu na kupelekwa Kituo cha Polisi Kijitonyama, Dar kwa mahojiano zaidi ambapo afisa mmoja amesema atafikishwa mahakamani wakati wowote.
No comments:
Post a Comment