WAENDESHA pikipiki za biashara, maarufu bodaboda mjini Iringa, wamemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emanuel Nchimbi kusikiliza kilio chao kinachotokana na kuadhibiwa ikiwemo kwa viboko na baadhi ya askari wa Usalama Barabarani.
Wakizungumza na gazeti hili katika kikao chao na waandishi wa habari jana, waendesha boda boda hao, bila kuwataja majina askari hao, wamewalalamikia kwa kuwanyanyasa wanapowakamata kwa makosa mbalimbali.
Baadhi yao wamedai wanaona ni bora warudi katika uhalifu kuliko kuendelea na biashara hiyo kwa kuwa wanapata bugudha kutoka kwa askari wa Usalama Barabarani.
Mwenyekiti wao, Mwambone Joseph, alisema bodaboda ndio njia pekee rahisi kwao iliyowapa ajira ya kudumu na jeshi hilo linajua kwamba vijana hao ndio wale waliohamasishwa kuondoka katika uhalifu na kutafuta shughuli zingine za kudumu.
Kwa mujibu wa Joseph, mbali na kuchapwa viboko kwa makosa ya barabarani ikiwemo kupakia abiria kwa staili inayojulikana kama mshikaki, wamekuwa wakiombwa rushwa wanaposahau kutembea na leseni ya udereva au na kofia ya abiria.
Alisema zaidi ya pikipiki 50 zimekuwa zikikamatwa kwa siku kwa sababu ya makosa hayo na kila moja hulipiwa faini ya Sh 30,000.
Mmoja wa madereva hao, Emanuel Joseph, alisema matrafiki wamewageuza vitega uchumi vyao na wanapokataa kutoa kitu kidogo, wanawakamata na kuwapeleka kituoni ili walipe faini ya Sh 30,000.
Alisema hawana kipingamizi wanapotakiwa kulipa faini hiyo, lakini kwa kuwa kila siku idadi kubwa kutoka miongoni mwao imekuwa ikikamatwa, wanataka kujua kiasi gani Polisi imepata tangu wameanza kukamatwa na jinsi wanavyozitumia.
“Hivi sasa Manispaa ya Iringa ina wastani wa bajaji 500; baadhi ya vijana wanaoziendesha walikuwa vibaka, wavuta bangi na walikuwa wakipanga kufanya uhalifu kila uchao,” alisema.
Badala ya kuendelea kuwakamata waendesha bodaboda hao, waliomba Jeshi la Polisi litumie hekima kwa kuwapa mafunzo maalumu ya udereva na usalama kwa gharama watakayokuwa tayari kuichangia.
Alhamisi ya wiki hii, waendesha pikipiki hao walitarajia kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba, ili wamuombe pia awasaidie kufikisha kilio chao walikokuita ‘ngazi za juu.’
No comments:
Post a Comment