MWANAMKE mkazi wa mkoani Mara ametoa ushuhuda wa namna vitendo vya ukatili kijinsia vilivyokithiri kwa kueleza namna alivyounguzwa kwa pasi na mumewe baada ya kukuta hakuna chakula nyumbani.
Aliutoa katika mdahalo wa kupinga ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali linalotetea haki za wanawake na watoto wa kike la Kivulini. Felista John alisema aliunguzwa na pasi katika mguu wake wa kulia na mumewe aliyetoka kazini na kukuta hakuna chakula nyumbani.
“Mimi ni mjasiriamali nauza mboga, siku ya tukio sikufanya biashara hivyo nilikosa hela kwa ajili ya kununua unga na mume wangu aliporudi nyumbani na kukuta hakuna chakula, alichukua pasi na kuniunguza kwa kushirikiana na nduguze,” alisema Felista.
Kutokana na kile alichosema ni ukubwa wa tatizo huku wanawake wakiendelea kufanyiwa ukatili, aliomba serikali kuziwezesha kiuchumi taasisi za raia ili ziweze kutoa elimu ya kupinga ukatili.
Kwa upande wake, askari polisi, Peter Kusaga kutoka Kata ya Kamunyonge wilayani Musoma, akichangia mada iliyohusu kupinga ukatili wa kijinsia, alitaka wananchi kujitokeza kwa wingi mahakamani kutoa ushahidi katika kesi za ukatili wa kijinsia ili wahusika waweze kutiwa hatiani.
Kusaga alisema hatua ya wananchi kujitokeza na kutoa ushahidi mahakamani, itasaidia katika kukomesha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike unaoendelea hivi sasa.
Akitoa mfano, Kusaga alisema hivi sasa wana kesi inayoendelea ya binti wa kidato cha pili kukatishwa masomo, lakini binti huyo amegoma kwenda kutoa ushahidi mahakamani kwani aliyembaka kwa sasa wanaishi naye kama mke na mume.
Hata hivyo, alisema kwa sasa vitendo vya ukatili vimepungua ikilinganishwa na siku za nyuma. Alisema hivi sasa wamekuwa wakipokea kesi tano kwa wiki zinazohusu ukatili wakati siku za nyuma zilikuwa zikizidi 10.
Akifafanua, alisema hivi sasa kesi tatu zipo mahakamani zinazohusisha matukio ya ubakaji katika maeneo ya Makoko, Nyakato na Mashikamano na kwamba mwaka jana kesi moja ya ukatili ilitolewa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela.
No comments:
Post a Comment