aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Saturday, August 24, 2013

MADINI YA BILIONI 13 YAKAMATWA UWANJA WA NDEGE..


SERIKALI kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini, imekamata madini ya vito yenye thamani ya Sh bilioni 13.17, yaliyokuwa mbioni kutoroshwa nje ya nchi. Madini hayo yalikamatwa katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini, ikiwa ni pamoja na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro na Mwanza. 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta, alisema madini hayo yalikamatwa kwa kipindi cha kuanzia Septemba 2012 hadi Julai, 2013.

Mteta alisema matukio ya utoroshwaji wa madini yamekuwa yakihusisha wageni zaidi, huku akitaja madini yanayoongoza kutoroshwa kwenda nje ni Tanzanite (vito), Amber, Green Gunnet, Soil and gold, Red gold moon stone na Green Tomalin.

Mteta alisema biashara ya kusafirisha madini nje ya nchi kwa njia za magendo, hivi sasa imeshamiri nchini na kuifananisha na biashara haramu ya usafirishaji wa dawa za kulevya.

“Biashara hii hufanywa sana na raia wa nje, hatukatai watu wasifanye biashara ya madini, lakini wafuate utaratibu unaokubalika.

“Zipo kesi zinaendelea mahakamani na kesi nyingine zipo mikononi mwa polisi kwa uchunguzi, lakini zipo kesi tatu tayari hukumu imetolewa na madini kutaifishwa,” alisema Mteta.

Mteta alisema Agosti 20, mwaka huu, raia mmoja wa kigeni (hakumtaja jina wala uraia), alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere akiwa na aina mbali mbali za madini yenye thamani ya Sh. milioni 25.32.

Mteta alisema siku hiyo hiyo, TMAA kwa kushirikiana na polisi walimkamata raia mwingine wa kigeni katika makazi yake, Jangwani Beach, akiwa na madini ya vito vya thamani.

“Uthaminishaji wa madini hayo unaendelea, japokuwa yanaonekana kuwa na thamani kubwa sana, mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Alisema TMAA ipo katika hatua za mwisho kuweka mtambo wa kisasa katika viwanja vyote vya ndege, utakaosaidia kubaini watu wanaotorosha madini kwenda nje ya nchi.

“Ni vigumu sana kubaini mtu akiwa amebeba madini, sababu hakuna sauti inayotoka pale mtuhumiwa anapopita kwenye mashine za usalama kwenye viwanja vya ndege, ikilinganishwa na dawa za kulevya au kitu cha hatari,” alisema.

No comments:

Post a Comment