aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Sunday, June 15, 2014

RAIS MPYA WA MALAWI KUOA WIKI IJAYO BAADA YA KUISHI MAISHA YA UKAPERA KWA ZAIDI YA MIAKA 30

Wiki mbili baada ya kuitwaa rasmi Ikulu ya Malawi, Rais mpya wa nchi hiyo, Profesa Peter Mutharika anatarajiwa kufunga ndoa na Gertrude Maseko Jumamosi ijayo, baada ya kuishi maisha ya ukapera kwa zaidi ya miaka 30.
 
Mutharika, mdogo wa Rais wa Pili wa Malawi, Bingu wa Mutharika ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa mume wa Christophine G. Mutharika, raia wa Visiwa vya Carribean na kubahatika kuzaa naye watoto watatu, Monique, Moyenda na Mahopela ambao wote ni wanasheria mahiri kwa sasa nchini Marekani.
 
Hata hivyo, Mutharika alimpoteza mkewe huyo kwa ugonjwa wa kansa mwaka 1990, hivyo kumfanya asioe kwa muda mrefu, huku akijikita zaidi katika kazi zake za uwakili kwa zaidi ya miaka 40 nchini Marekani.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Malawi iliyosainiwa na Mwandishi wa Habari wa Rais, Chikondi Juma imeeleza kuwa ndoa ya Rais Mutharika na Maseko itafungwa Jumamosi ya Juni 21 mwaka huu katika Kanisa la Mtakatifu Michael na Malaika Wote, jijini Blantyre.
 
Harusi hiyo inafanyika huku Wamalawi wakifanya chereko za kuwasili kwa mara ya kwanza nchini Malawi kwa mabinti wa rais huyo, Monique na Moyenda, siku chache baada ya uchaguzi uliomwingiza Ikulu baba yao akiwa Rais wa Tano wa nchi hiyo.
 
Taarifa hiyo ya Ikulu imeongeza kuwa, Maseko ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Balaka Kaskazini kwa tiketi ya chama cha Democratic Progress (DPP) cha Mutharika, ni mwandani wa muda mrefu wa Rais mpya na kwamba alikuwa sambamba naye katika kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 20, mwaka huu na kuhitimisha utawala wa miaka miwili na ushee wa Rais Joyce Banda.
 
“Baada ya shughuli za kanisani, chereko zitahamia katika familia ya Mutharika iliyopo Ndata katika Wilaya ya Thyolo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
 
Tukio la kuoa na kuwasili kwa watoto wake, kumeelezwa kumaliza uvumi uliokuwa umeenezwa na wapinzani wake kisiasa kuwa, Mutharika hakuwa mwanamume aliyekamilika.
 
Uvumi huo ulijibiwa na Katibu Mkuu wa DPP, Chimwemwe Chipungu mara baada ya kuwapokea mabinti hao kwenye Uwanja wa Ndege wa Lilongwe wakitokea Marekani, akisema: “Watu walikuwa na hofu kama Rais Mutharika ana watoto. Ni uvumi wa kijinga. Waliokuwa wakieneza uvumi huo sasa watapata aibu. Rais wetu ana watoto na ni baba wa familia.”
 
Na Rais Mutharika mwenyewe, wakati wa kampeni aliyasigina maneno ya wapinzani wake kwa kusema ana watoto wenye afya njema, akili timamu na wanasheria maarufu Marekani, mmoja akiwa Profesa katika moja ya vyuo vikuu vya huko.
 
“Ukiachana na watoto, pia nina wajukuu kadhaa,” alisema Mutharika mwenye umri wa miaka 74 sasa ambaye akiwa mwanazuoni katika masuala ya sheria, aliwahi kufundisha katika vyuo kadhaa, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika miaka ya 1970.
 

Kabla ya kuutwaa urais wa Malawi, Profesa Mutharika aliyebobea katika masuala ya sheria ambaye pia ni mwanasiasa mzoefu na mashuhuri, ameshika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali zikiwamo Wizara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nafasi aliyoishika hadi anaingia katika uchaguzi mkuu hivi karibuni.