aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Tuesday, June 3, 2014

MSIBA WA TYSON MAJENEZA MAWILI

 Kwenye gari ni moja ya jeneza lilikusudiwa awali kutumika kwa ajili ya kuuhifadhi mwili wa marehemu George Otieno,' Tyson'.

HUKU akiacha wake watatu, Yvonne-Sheryl  Ngatikwa ‘Monalisa’, Beatrice na Lucy, msiba wa marehemu George Otieno ‘Tyson’ (41) umezua maajabu kwa kuwa na majeneza mawili,

Kwa mujibu wa chanzo, uwepo wa majeneza hayo ulitokana na kukosekana kwa usimamizi imara kiasi cha kuyafanya yakosolewe kwa kukosa ubora kulingana na hadhi ya marehemu na hivyo nusura linunuliwe la tatu.
Msanii wa Bongo Fleva, Ambwene Yesaya ‘AY’ akijitolea shilingi laki sita kufanikisha ununuzi wa jeneza la pili.
JENEZA LA KWANZA
Jeneza la kwanza lilikuwa la mbao bila ishara kwamba ni jeneza. Wengi waliliita sanduku kutokana na muundo wake na lilifikishwa hospitali tayari kwa kuubeba mwili wa marehemu.
JENEZA LA PILI
Msanii wa Bongo Fleva, Ambwene Yesaya ‘AY’ alipofika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro alishtushwa kuwepo kwa jeneza hilo hivyo alijitolea kwenda kununua jingine kwa gharama ya shilingi 600,000.
Jeneza la pili likichukuliwa tayari kwa kuuhifadhi mwili wa marehemu Tyson.
MCHANGO MKUBWA
Akizungumza na Uwazi juzi, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ‘Taff’, Simon Mwakifwamba alikiri kuwepo kwa majeneza mawili lakini akasema AY aliokoa jahazi kwa kununua la pili lenye ubora.
Hata hivyo, baada ya jeneza la pili kuufikisha mwili kwenye Hospitali ya Kairuki jijini Dar, wasanii wa Bongo Movie walilipinga wakidai nalo pia halikuwa na hadhi ya kubebea mwili wa Tyson hadi Kisumo, Kenya ambako marehemu atazikwa.
“Lile jeneza alilonunua AY nalo si bora sana ukilinganisha na majeneza ya marehemu Adam Kuambiana na Recho Haule. Tyson si mtu wa kumweka kwenye jeneza kama hili. Tutatafuta jingine lakini tutamwambia AY atusamehe,” alisema Katibu wa Bongo Movie, William Mtitu.
Marehemu George Otieno,' Tyson' enzi za uhai wake.
Naye Mwakifwamba akizungumzia kuhusu kununua jeneza jingine na kuachana na lile lililosafirishia mwili kutoka Morogoro, alisema:
“Kikao cha mwisho tumekubaliana kwamba, jeneza litumike lilelile la Morogoro ila lifanyiwe decoration (mapambo) ili liweze kuwa la kisasa zaidi.”
MKUU WA WILAYA
Mwakifwamba alikwenda mbele zaidi kwa kusema, AY mbali na kununua jeneza lakini pia alinunua shati jipya la marehemu kufuatia T-shirt aliyoivaa siku ya ajali kujaa damu.
Akaongeza: “Wa kuwashukuru ni wengi, mfano Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka yeye ndiye aliyetoa usafiri wa gari (Toyota Land Cruiser) kwa ajili ya kuleta mwili wa marehemu hapa Dar.”
MWILI KUSAFIRISHWA KENYA
Naye ndugu wa marehemu Tyson, Felix Owino alipozungumza na Uwazi juzi alisema kikao cha familia kimeamua kuusafirisha mwili kwenda kuzikwa Kisumo, Kenya.
Alisema mwili utasafirishwa Jumanne (leo) au Jumatano kulingana na kukamilika kwa bajeti ambayo ni shilingi milioni 19. Aliongeza kuwa, mwili huo utaagwa kwenye Viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.
Marehemu Tyson alifariki dunia kwa ajali ya gari aina ya Toyota Noah, Ijumaa iliyopita wakati yeye na wenzake wakitokea Dodoma kwenda Dar. Wengine watatu walijeruhiwa na wanatibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, akiwemo MC maarufu, Gladness Chiduo ‘Zipompa’.
Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Gairo kuelekea Morogoro. Marehemu ameacha watoto wawili.

No comments:

Post a Comment