Mwanamke Yasinta Rwechengura, mkazi wa Boko wilayani Kinondoni, Dar anayekabiliwa na kesi ya kutuhumiwa kumtesa hausigeli wake kwa miaka miwili (siku 730), amejikuta akihenyeshwa mahakamani.Hayo yamemkuta juzi alipofikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Kinondoni kujibu tuhuma zinazomkabili ambapo alikuwa akipokea amri kutoka kwa askari na kumfanya kukosa raha.
Msala huo unagusa hisia za wengi ndiyo maana watu kutoka viunga mbalimbali vya Jiji la Dar walifurika mahakamani hapo kusikiliza mwenendo wa kesi hiyo iliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Boniphace Lihamwike.
Akisoma kesi hiyo mahakamani hapo, wakili wa serikali ambaye alikuwa upande wa jamhuri, Mohamed Salum alisema anaiomba mahakama hiyo kutotoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa sababu za kiusalama.
Sababu ya pili alisema bado hali ya mgonjwa ni mbaya na amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kesi hiyo ambayo inafuatiliwa kwa ukaribu na wanaharakati wa haki za binadamu, awali ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Suleiman Mzava ambaye juzi hakufika mahakamani hapo kutokana na uhamisho alioupata na badala yake kesi hiyo ilitajwa kwa Hakimu Lihamwike.
Upande unaomtetea mtuhumiwa huyo uliokuwa ukiongozwa na wakili wa kujitegemea, Msomi Gidion, uliiomba mahakama kumpa mteja wao dhamana lakini ukagonga mwamba.
Hata hivyo, wakili Mohamed aliendelea kuiomba mahakama kwa mara nyingine kutotoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa sababu alizozitoa awali.
Hata hivyo, wakili Mohamed aliendelea kuiomba mahakama kwa mara nyingine kutotoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa sababu alizozitoa awali.
Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema pande zote zilikuwa na hoja akianza na upande wa mtuhumiwa ambapo alitoa ufafanuzi kuwa ni haki yake ya kikatiba kupata dhamana lakini upande wa jamhuri nao ulikuwa na hoja.
Hakimu huyo alisema kuwa shauri hilo kwa mara ya kwanza lilianzia kwa hakimu mwingine na ndani ya faili la kesi hiyo hakukuwa na vielelezo vyovyote hivyo kuirudisha kesi hiyo kwa hakimu kiongozi kwa ajili ya kupangiwa hakimu atakayeisikiliza.
Baada ya hapo, mtuhumiwa alipandishwa kwenye karandinga na kurudishwa mahabusu kwenye Gereza la Segerea, Dar kuendelea kuhenya hadi atakapopata dhamana huku wananchi waliofika mahakamani hapo wakimshangaa.
No comments:
Post a Comment