aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Tuesday, September 3, 2013

JINSI MABOSI WANAVYOTUMIA VYEO KULAZIMISHA NGONO OFISINI

KWA UFUPI

Mabosi huwatafutia safari kama njia ya kuwanasa kwa kuwa wanapokuwa hotelini pekee, wanawake wengi wanakosa ujasili wa kukataa.


Wengine hutoa ofa kama vile kupandishwa vyeo, kununulia magari au hata safari za nje.Wengi wanaofanya haya ni waume za watu, wengine ukitajiwa ni ngumu kuamini kwa namna wanavyoonekana wana hekima usoni au mavazi yao.




Licha ya harakati mbalimbali za kumkomboa mwanamke, bado kuna mabosi nchini wanawanyanyasa wanawake kwa kuwalazimisha kufanya nao ngono.

Wapo wanaonyanyaswa au hata kuteswa ikiwemo kusemwa maneno machafu au kutishiwa kufukuzwa kazi kwa sababu tu wamekataa kutoa penzi kwa bosi.

Wale wanaokubali, wengine wanaishia kupewa ahadi hewa za kufundishwa magari, kupelekewa kozi mbalimbali. Hata hivyo mbaya zaidi ni kwamba mabosi wengine hata kama wameoa, hupenda kuwamiliki wanawake hao kana kwamba ni wake zao kwa kuwafuatilia sana nyendo zao.

Ukahaba wa mabosi hufanywaje?

Baadhi ya wanaume kwa mwonekano ni vigumu kuamini kama ndiyo wanaofanya vitendo vichafu kwa wafanyakazi wao. Wanaposimama kwenye vikao, utasema mtu huyu, lakini wafanyakazi wa kike wamekuwa ni wenye kuwanyanyasa mno.

Baadhi ya mabosi wamekuwa wakitoa vitisho kuwa ‘kama hunipi penzi nitakuporomosha cheo au hata kukufanyia visa vyovyote hadi uhame’.

Katika baadhi ya ofisi badala ya mabosi kutumika kama washauri wa wafanyakazi wao kuzipenda ndoa na nyumba zao, ndio wamekuwa wakitumia fedha zao kuwahonga wanawake hata magari, huku makatibu muhtasi wakidaiwa kuwa ndio wanaosumbuliwa zaidi.

Wapo mabosi huwaingia wanawake wakiwemo wake za watu kwa kuwapangia safari za mikoani au nje ya nchi hasa wanapoona hawana wepesi wa kukubaliana na matakwa yao.

“Nakumbuka kuna bosi mmoja katika ofisi moja nyeti aliwahi kudaiwa kumnunulia gari mke wa mtu kabla ya kuhama chombo hicho,” anasema mkazi mmoja wa Kimara.

Bosi aliweza kumpa safari ya nje mwanamke na kisha kumnunulia gari zuri kuliko la mumewe.

Hii ni moja ya kati ya matukio mengi ya mabosi kuwaingiza wafanyakazi wao katika ngono badala ya kuwa ndio washauri wema kwa wafanyakazi ili waweze kuziheshimu ndoa zao.

Sifa zifaazo kwa mabosi


Kwa mujibu wa msomi maarufu katika tansia ya uongozi, Christopher Rocchio wa Marekani, katika chapisho lake la ‘Secret Millionaire’, mabosi wanapaswa kutoa miongozo mizuri ya namna ya kuishi vema ndani na nje ya sehemu za kazi, kwa bahati mbaya, baadhi yao wamekuwa sababu ya kuharibika kwa ndoa za wafanyakazi wao.

Wataalamu wengine katika masuala ya uongozi na utawala, Ruth Faulkner katika chapisho lake la “Viridor boss’ na Fernandez, Maria-Elena katika gazeti la Los Angeles Times, mabosi wanaweza kuchangia kuharibu au kujenga ndoa za wafanyakazi wao kutokana na mafundisho au namna wanavyoendesha mambo sehemu za kazi.

Je, wewe ni bosi wa namna gani au ofisini kwenu mabosi wenu wakoje? Kila mtu aliyeko kwenye ajira analo jibu lake. Hata hivyo kwa vyovyote inavyokuwa ni suala la msingi kila bosi kutafakari kwamba dhamana aliyonayo si kufanya ngono wala kutongoza wafanyakazi na kuwatisha, bali kushirikiana nao kuongeza mafanikio katika eneo la kazi.

Simulizi ya mmoja wa wanawake 

Mwajuma Sabuni (sio jina lake halisi), ni mfanyakazi katika kiwanda kimoja jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) analalamikia unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wenye vyeo vya juu yao.

“Nimefanya kazi katika kiwanda hiki kwa miaka saba sasa. Sisi wafanyakazi wa kike imekuwa ni kawaida kulazimishwa kufanya ngono.Baadhi ya wasimamizi wa vitengo ndio wahusika wakuu wa kulazimisha wapewe ngono, ukiwakataa ajira yako inakuwa hatarini”.

Haya ni baadhi ya mambo mabaya wanayofanyiwa wanawake sehemu za kazi.

Baadhi yao hulazimika kujiingiza kwenye ngono zisizo salama kwa sababu tu wanaogopa kuwaambia mabosi wao watumia kinga kwa hofu kwamba itaonekana kama ni kuwadhalilisha kuwa huenda wana Ukimwi. 

Katika mkutano wa wadau wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wanawake wako kwenye hatari zaidi ya kuathirika na ugonjwa huo kwa sababu baadhi ya hao mabosi hawatumii kinga na huwa hawako tayari kupima, kwa bahati mbaya zaidi wale wanaofanya nao baadhi yao huogopa kuhoji chochote hivyo mabosi hufanya watakavyo ikiwemo kutotumia kinga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), Dk Fatma Mrisho anasema, “Hatari ya wanawake kuathirika na Ukimwi ni kubwa mno. Pia ni changamoto kubwa inayohitaji jitihada za kila mmoja wetu.”

Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Hezron Kaaya anapendekeza mifuko ya hifadhi ya jamii kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wanawake na wasichana.


Mkurugenzi wa Sera na Utetezi wa Chama cha Waajiri nchini (ATE), Justina Lyela ambaye amewataka waajiri nchini kuepuka kuwapunja wafanyakazi wa kike ukilinganisha na wanaume ili kuwawezesha kiuchumi.Tamwa na unyanyasaji
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), katika moja ya mpango mkakati wake wa miaka mitano 2010-2014, pamoja na mambo mengine kimepanga kufanya shughuli ambazo zitaimarisha elimu kwa mtoto wa kike kwa kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Unyanyasaji wa kijinsia

Unyanyasaji wa kijinsia ni tendo baya kwa haki za binadamu na linasababisha maumivu kwa wahusika. Vilevile, linahusisha kumlazimisha mtu kufanya nae mapenzi bila ridhaa yake. Lakini kufanya mapenzi na watu kama baba, mama, kaka, dada, babu au bibi ni aina nyingine ya unyanyasaji wa jinsia.

Unyanyasaji wa kijinsia ni kosa la jinai. Unyanyasaji huo ni pamoja na kutumia maneno kwa mfano baadhi ya mabosi huwatishia wafanyakazi wa kike kwamba wasipokubali kufanya nao ngono watawafukuza kazi.

Unyanyasaji sio unahusisha sauti, ishara au maonyesho ya sehemu za mwili kwa makusudi kinyume na matakwa ya mtu, kwamba kwa mfano mtu anaweza kukuonyesha sehemu za siri au kukuvamia kwa kugusa sehemu zako za siri kama njia ya kukushawishi mfanye ngono.

Kanuni za adhabu (sura ya 16) kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, zipo wazi kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kujamiiana na mtu mwingine bila ya ridhaa yakeƖ.anayefanya hivi maana yake ni sawa na ubakaji.

Ni kosa kupigwa busu bila ridhaa

Sheria ziko wazi kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kushika viungo vya siri vya uzazi, au kukupiga busu bila ya ridhaa ya mhusika.

Hivi karibuni, Tamwa ilizindua ripoti ya utafiti wa unyanyasaji wa kijinsia uliofanyika Aprili mwaka huu katika wilaya 10 za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mkurugenzi wake, Valery Msoka anasema waafiti waliwahoji watu mbalimbali katika ngazi za familia na kupata ukweli wa hali halisi ya unyanyasaji wa kijinsia.

W i l a y a zilizofanyiwa utafiti ni Wete (Pemba Kaskazini), Mjini Magharibi (Unguja Magharibi), Unguja Kusini, Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Mvomero (Morogoro), Lindi vijijini na Ruangwa (Lindi), Kinondoni na Ilala, Dar es Salaam.Kwa mujibu wa Tamwa matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia kwa ujumla yameshamiri nchini, na kwamba zaidi ya asilimia 39 ya wanawake nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili.
Watuhumiwa wa unyanyasaji huu kwa kiwango kikubwa ni wanaume, huku sheria zikionekana kushindwa kuchukua mkondo wake ipasavyo.

Mfano halisi ni ripoti ya Polisi Zanzibar, ambayo inasema katika mwaka 2011, yalikuwapo matukio 268 ya unyanyasaji yaliyoripotiwa, kesi zilizofikishwa mahakamani ni 55, hata hivyo ni kesi moja ndiyo iliyomtia mtuhumiwa hatiani.

Je, nini kifanyike kuepusha mateso wanayofanyiwa wanawake maofisini? Ni changamoto ambayo inapaswa kuendelea kufanyiwa kazi ili kuepusha mabosi viwembe wanaoendelea kuwanyanyasa wanawake wakitumia madaraka yao.

Waziri Sophia Simba wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ametaka kuwepo usawa wa fursa kama vile elimu na rasilimali za uchumi hasa kwa wanawake.

Waziri Simba anaamini kwamba kwa jitihada ambazo Serikali inaendelea nazo nchini, tatizo la unyanyasaji wa kijinsia litaendelea kupungua.

Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na uwepo wa sheria mbalimbali ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaonekana kushawishi watu kujali haki za kijinsia. Chanzo: Mabosi wanavyotumia vyeo kulazimisha ngono - Habari Ya Ndani - mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment