aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Tuesday, September 24, 2013

AL-SHABAAB WATISHIA KUIVAMIA TANZANIA NA UGANDA.....DCI MANUMBA ASEMA TUMEJIPANGA KUKABILIANA NAO....!!



Wakati wa Jeshi la Polisi la Tanzania likisema linafuatilia taarifa za vitisho za kundi la Al-Shabaab la Somalia za kushambulia, Mtanzania mmoja, Vedasto Nsanzugwanko ambaye alijeruhiwa kwenye shambulio la Kenya ameelezea yaliyomkuta. 

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba alisema jana kuwa wameanza kufuatilia kwa undani taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kwamba kundi la Al-Shabaab linajipanga kuishambulia Tanzania na Uganda.
 

DCI Manumba alikiri kusikia taarifa hizo na kusema kuwa Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi wa kina: “Siwezi kukueleza ni uchunguzi wa aina gani tutakaofanya, hiyo ni siri yetu.”
 

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Meja Eric Komba alisema kuwa kuna uwezekano taarifa hizo zikapikwa na wajanja wachache kwa ajili ya kuwajengea hofu wananchi.
 

“Taarifa za kwenye mitandao wakati mwingine ni uzushi mtupu… kuna kipindi ziliwekwa taarifa za uongo zinazohusu jeshi hili,” alisema.
 

Alipotakiwa kutoa msimamo wa jeshi hilo iwapo taarifa hizo zitakuwa na ukweli alisema, “Jeshi tuko tayari kwa jambo lolote.”
 

Mtanzania ajeruhiwa
 
Nsanzugwako ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Kulinda Watoto kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watoto (Unicef), Kenya alisema kwamba akiwa katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi alipigwa risasi miguu yote miwili.
 

Alisema alifikwa na mkasa huo baada ya kupitia katika maduka hayo akitokea kazini ili kupata kahawa... “Nilipofika baada ya nusu saa nilisikia milio ya risasi ndipo nikaona purukushani zimeanza.”
 

Nsanzugwako alisema alianza kukimbia na wenzake huku wakijaribu kuokoa watoto waliokuwepo katika eneo hilo ambao walikuwa katika shindano la mapishi lililoandaliwa na Radio Africa Group.
 

“Watoto walianza kukimbilia ghorofa za juu zaidi na magaidi walianza kuwafuata.
 

“Baada ya hapo, waliendelea kutukimbiza na nilikutana nao ana kwa ana na mmoja wa magaidi hao ambaye alinifyatulia risasi na kunipiga miguu yote miwili,” alisema.


Alieleza kwamba alijikongoja hadi alipofanikiwa kutoka nje kwa kupitia mlango uliokuwa mbele yake na kupokewa na polisi na kisha kuchukuliwa na Msalaba Mwekundu kwa ajili ya huduma ya kwanza na kisha kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

“Jioni yake nilitakiwa kusafiri kwenda Geneva, Uswisi kikazi lakini kutokana na tukio hilo nilishindwa kufanya hivyo,” alisema.

Alisema amekuwa jijini Nairobi kwa miezi saba akiwa anafanya kazi Unicef.

Kaka wa majeruhi huyo, Mbunge wa zamani Kasulu Mashariki, Daniel Nsanzugwako, alisema amekuwa akiwasiliana na mdogo wake huyo na kwamba anaendelea vyema.

Nsanzugwako, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo alisema mdogo wake alimweleza kuwa tayari ameshafanyiwa upasuaji lakini bado hajaweza kutembea.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, Shiyo Innocent ilithibitisha kuwapo kwa Mtanzania mmoja ambaye amejeruhiwa kwa risasi katika miguu yake yote... “Ubalozi unaendelea kufuatilia kama kuna Watanzania wengine waliokuwepo kwenye tukio hilo.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule alisema Serikali inaendelea kufuatilia afya ya Mtanzania huyo.

“Ofisi yetu ya ubalozi iko karibu na inafuatilia kila kinachoendelea. Kwa sasa nimeambiwa kuwa majeruhi anaendelea vizuri na tuna matumaini atapata ahueni,” alisema.

-Mwananchi

No comments:

Post a Comment