aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Monday, September 30, 2013

Majeshi ya Tanzania yana kiwango kikubwa cha ubora – Ban Ki Moon

jakaya-mrisho-kikwete-ban-ki-moon-2011-9-21-19-0-32
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Ban Ki Moon kwenye picha ya pamoja na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.(Picha na Maktaba).
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Ban Ki Moon amemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Umoja wa Mataifa unajivunia mchango na ushiriki wa majeshi ya Tanzania katika Brigedi ya Kimataifa ya Kutuliza Hali (FIB) katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mheshimiwa Ban Ki Moon amesema kuwa majeshi ya Tanzania katika DRC, kama ilivyo katika sehemu mbali mbali duniani yanapolinda amani, yamethibitisha ubora wa kufanya kazi katika Congo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amempa Rais Kikwete salamu za rambirambi na pole nyingi kuomboleza vifo vya wanajeshi tisawaliokuwa wanalinda amani chini ya Umoja wa Mataifa katika Darfur, Sudan, ambako Julai mwaka huu wanajeshi saba walipoteza maisha na katika Congo ambako wawili wamepoteza maisha.
Katibu Mkuu Ban Ki Moon ameyasema hayo leo, Ijumaa, Septemba 27, 2013, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa UN mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete alikuwa mjini New York kuhudhuria Mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo alilihutubia baadaye leo mchana. Rais ataondoka kesho,  Jumamosi, Septemba 28, 2013 kurejea nyumbani baada ya ziara hiyo ya kikazi.
Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Ban Ki Moon amemwambia Rais Kikwete: “Nakushukuru kwa uongozi wako na kwa uamuzi wako wa kukubali kushiriki katika kundi la Eleven plus Four la kutafuta suluhisho katika DRC. Ndani ya DRC lenyewe, Jeshi la Tanzania limethibitisha kuwa jeshi linaloleta tofauti, lenye ubora uliothibitika ndani ya FIB. Tunakushukuru sana kwa kushiriki ulinzi wa amani duniani.”
Ameongeza Mheshimiwa Ban Ki Moon: “Lakini pia nataka kuelezea rambirambi zangu na pole nyingi kwako kutokana na gharama kubwa ya maisha ambayo majeshi ya Tanzania katika Darfur Julai mwaka huu na majuzi katika DRC yamepata. Ni dhahiri kuwa wewe kama kiongozi unaelewa fika maana ya amani ya dunia na faida zake.”
Tanzania ina zaidi ya wanajeshi 2,500 wanaolinda amani katika Darfur, Sudan; katika DRC na katika Lebanon na ni nchi ya sita katika Afrika katika uchangiaji wa wanajeshi na polisi wa kulinda amani duniani na inashikilia nafasi ya 12 duniani.
Baada ya hapo, Mheshimiwa Ban Ki Moon ametaka kujua mambo kadhaa kutoka kwa Rais Kikwete ikiwa ni pamoja na jinsi mchakato wa Katiba Mpya unavyoendelea na kuitakia Tanzania mafanikio katika mchakato huo, uhusiano na majirani hasa Rwanda na kushauri uhusiano huo uboreshwe, hatua zinazochukuliwa kukomesha vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) na hatimaye akamwalika Rais Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Duniani ambao utajadili Mabadiliko ya Tabianchi mwakani wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la UN.
Rais Kikwete amemshukuru Katibu Mkuu Ban Ki Moon kuhusu rambirambi za Tanzania kupoteza wanajeshi wake katika Sudan na Congo akisititiza kuwa Tanzania inayo wajibu wa kushirikiana na Jumuia ya Kimataifa katika kulinda amani katika sehemu mbali mbali na kuwa inaelewa fika athari na hatari za shughuli za kulinda amani duniani.
Rais pia amemweleza Katibu Mkuu huyo wa UN kuhusu uhusiano wa Tanzania na Rwanda akisisitiza kuwa kufuatia mkutano wa Kampala, Uganda, kati yake na Rais Paul Kagame wa Rwanda anaamini kuwa sasa uhusiano huo utarejea katika hali yake ya udugu wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili.
Kuhusu mauaji ya albino, Rais Kikwete amesema: “Tumelijadili suala hili mara kadhaa huko nyuma Mheshimiwa Katibu Mkuu na kama nilivyopata kukuambia hili ni tatizo ambalo chimbuko lake ni imani za ushirikina na uchawi. Ni imani za kijinga tu.”
Ameongeza: “Kama unavyojua, tuliendesha kura ya maoni kubaini washiriki wa ujinga huu. Kufuatia kura hiyo, tulikamata watu, wakafikishwa mahakamani na wengine wamehukumiwa kifo. Lakini ni jambo ambalo sasa limepoa sana nchini kwetu.”

No comments:

Post a Comment