Askari huyo ambaye jina lake halikutajwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama, wakati wavamizi hao wanavamia jengo hilo siku ya Jumamosi, naye alikuwemo ndani ya jengo hilo akinywa kahawa.
Kwenye baadhi ya mitandao, askari huyo ameonekana akiwasaidia wanawake wawili huku akiwa ameweka bastola kwenye suruali yake, ingawa sura yake imefichwa.
Habari zinasema kuwa, askari huyo ameonekana shujaa kwani licha ya hali tete iliyokuwa ndani ya jengo hilo, aliweza kuingia na kutoka zaidi ya mara 12 akiwaokoa baadhi ya watu waliokwama ndani ya jengo hilo lenye maduka na migahawa mbalimbali.
“Alichofanya ni kitendo cha kishujaa sana, alikuwa akinywa kahawa na baadhi ya rafiki zake wakati wavamizi walivyoingia.
Alirudi ndani mara 12 na kufanikiwa kuokoa zaidi ya watu 100. Fikiria kuthubutu kurudi ndani huku akijua kabisa jinsi hali ilivyo ndani ya hilo jengo,” baadhi ya mashuhuda walinukuliwa.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, askari huyo wa Uingereza anafanya zaidi shughuli zake Kenya na nje ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia raia wa nchi yake wanaojishughulisha na mambo mbalimbali.
Agosti mwaka huu, gazeti la Daily Mirror liliripoti kuwa kikosi maalumu cha SAS na askari maalumu wa kupambana na ugaidi, wameanza kumtafuta Samantha Lewthwaite, Mwanamke anayetajwa kuwa ni raia wa Uingereza anayedaiwa kuwa gaidi ambaye pia anashirikiana na kundi la Al-Shabaab.
Mwanamke huyu mjane anayetajwa kuwa ni gaidi, inasemekana pia alishiriki kupanga na kutekeleza uvamizi mjini Nairobi.
Kikosi hicho cha SAS, kinaelezwa kuwa kinafanya kazi kwa ukaribu na vikosi vya ulinzi vya Uingereza, Kenya na vile vya nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Habari juu ya askari huyo zimekuja wakati milio ya risasi ikizidi kusikika ndani ya jengo hilo, huku maofisa wa usalama wa nchi hiyo wakisema kuwa wamedhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo. Habari zaidi zinasema kuwa, bado zaidi ya watu 10 wanashikiliwa ndani ya jengo hilo kama mateka.
No comments:
Post a Comment