aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Thursday, September 26, 2013

TANZANIA NA BURUNDI WAICHARUKIA EAC....WATAKA MAELEZO YA KINA KUTOKA RWANDA UGANDA NA KENYA...!!



HALI ya mambo imezidi kuwa tete katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya Tanzania na Burundi kutaka maelezo ya kina kutoka kwa nchi nyingine tatu wanachama za Kenya, Uganda na Rwanda zilizoanzisha ushirikiano mpya kinyemela kati yao, kwa kuzitenga nchi hizo mbili. 
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayoashiria kuwa Tanzania na Burundi zimetengwa na nchi hizo tatu ambazo zimeanzisha ushirikiano mpya kati yao kinyemela, kinyume cha mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo mwaka  1999.
Jumuiya ya sasa ilizaliwa tena upya Novemba 30, mwaka 1999 ikishirikisha nchi za Tanzania, Uganda na Kenya, wakati Rwanda na Burundi zilikaribishwa baadaye mwaka 2008.
Jumuiya hiyo mpya ilizaliwa baada ya ile ya awali iliyoanzishwa mwaka 1968 kuvunjika mwaka 1977 kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kushindwa kuelewana kwa wakuu wa nchi wanachama kwa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Jommo Kenyatta (Kenya) na Idd Amin (Uganda).
Habari za hivi karibuni zilizopatikana kutoka ndani ya EAC zinabainisha kwamba Tanzania na Burundi zimekerwa na hatua ya nchi wanachama wenzao za Kenya, Uganda na Rwanda kuanza mchakato wa kuanzisha shirikisho la kisiasa bila ya kuzishirikisha nchi hizo.
Tanzania na Burundi zinaelezwa kuwa kupitia kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Agosti 31, mwaka huu, mjini Arusha zilimtaka Mwenyekiti wa Baraza hilo, Shem Bageine, kutoka Uganda kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua za nchi hizo tatu kufanya mambo ambayo yanakwenda kinyume cha mkataba wa Jumuiya hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa hata hivyo Bageine hakuwa na majibu muafaka kuhusu hatua hiyo na ndipo nchi hizo mbili zilipoazimia kuhitaji majibu ya kina zaidi kuhusu suala hilo katika kikao kijacho kitakachofanyika Novemba, mwaka huu.
Pamoja na suala la kuanzisha mchakato wa shirikisho la kisiasa, nchi hizo tatu pia zinaelezwa kukubaliana kuanzisha ushirikiano katika eneo la kukusanya kodi  (single costumes territory).
Masuala mengine ambayo yanaelezwa kutozifurahisha nchi za Tanzania na Burundi ni hatua yao ya kukubaliana kuwa na visa moja kwa watalii watakaotembelea nchi hizo, kuimarisha miundombinu hasa ujenzi wa reli kutoka Bandari ya Mombasa-Kenya hadi Kigali Rwanda kupitia Kampala-Uganda.
Moja wa maofisa wa EAC ambaye ni Mtanzania (jina linahifadhiwa) alilimbia gazeti hili la Raia Mwema kuwa hali ndani ya sekretarieti ya jumuiya hiyo ni mbaya na hata watumishi kutoka nchi za Tanzania na Burundi wameanza kutengwa na wenzao.
“Kumekuwa na kutokuaminiana miongoni mwa maofisa wa juu katika jumuiya yetu, watumishi wa Tanzania ni kama tunatengwa na wenzetu,” alidai mtumishi huyo bila ya kufafanua zaidi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mwezi uliopita Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya EAC, Dk. Richard Sezibera, alikanusha madai kuwa hali si shwari ndani ya Jumuiya anayoiongoza.
 Dk. Sezibera alikaririwa akisema: “Hali ni shwari katika jumuiya na kila kitu kinakwenda vizuri kulingana na mkataba wa jumuiya tofauti zinazojitokeza ni za kawaida katika jumuiya yoyote ile ya watu kutofautiana mawazo.”!
Taarifa zinaeleza kuwa katika utetezi wake, Bagaine ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki nchini Uganda, aliwaeleza washiriki wa kikao hicho kuwa mikutano iliyowakutanisha viongozi wakuu wa nchi hizo tatu iliratibiwa na wizara za mambo nje katika nchi husika.
Waziri huyo alieleza kuwa kwa kawaida mikutano inayohusiana na masuala ya Afrika Mashariki huratibiwa na wizara husika katika kila nchi, lakini kwa suala hilo ilikuwa kinyume hivyo asingekuwa na majibu muafaka.
“Kutokana na mgongano uliojitokeza ujumbe wa Tanzania ulitaka upewe maelezo yanayotosheleza katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri kinachotarajiwa kufanyika mapema Novemba, mwaka huu, kabla ya kikao cha wakuu wa nchi ambao watakutana Novemba 30,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Akizungumzia mzozo huo aliyekuwa Waziri wa kivuli wa Afrika Mashariki kutoka Kambi Upinzani Bungeni- CHADEMA, Mustafa Akonaay, alisema ilikuwa mapema kwa nchi wanachama waanzilishi wa jumuiya kuziruhusu Rwanda na Burundi kujiunga na jumuiya hiyo.
“Hizi nchi mbili zilikuwa na matatizo ya ndani ya kiutawala baada ya kupigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu, hivyo ilikuwa ni mapema sana kuziruhusu kujiunga na jumuiya wakati bado zina matatizo ya ndani,” alieleza Akonaay.
Naye mwanzuoni maarufu katika diplomasia, Profesa Abdallah Safari, anasema katika msuguano huo kuna taarifa za muda mrefu kuwa baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika Mashariki wanataka kuharakisha shirikisho la kisiasa kwa maslahi yao wenyewe.
“Tetesi kuhusu suala hilo ni za muda mrefu na kulikuwa na mipango ya kupanua kitu kinachoitwa dola ya Wahima (Hima Empire) katika eneo la Maziwa Makuu hadi Tanzania, kuna uwezekano mipango hiyo bado iko vichwani mwa viongozi hao,” anasema Profesa Safari.
Anaongeza kusema; “Wakati mwingine sisi Watanzania ni chanzo cha kuanza kutengwa na wenzetu kutokana na kushamiri kwa tabia ya urasimu, uzembe na wizi katika sekta mbalimbali za umma na hata kushindwa kwenda sambamba na wenzetu ambao wanadhamira ya kufanya mambo kwa weledi zaidi.”!
Akitoa mfano Profesa huyo anasema katika sekta ya biashara Tanzania imeshindwa kuondoa urasimu katika Bandari ya Dar es Salaam kiasi cha wafanyabiashara kutoka nchi jirani wanaoitumia kusafirisha bidhaa zao kupata hasara. 
“Mlolongo  huo wa mambo yasiyo na msingi unasababisha usumbufu kwa wafanyabiashara wengi wanaopitisha bidhaa zao katika ardhi ya Tanzania na bidhaa hizo hupanda bei marudufu katika masoko zinakopelekwa na hivyo kuongeza gharama kwa watumiaji,”!
Katika hatua nyingine, alidai hatua ya Tanzania kuanza kutengwa inatokana na uongozi dhaifu wa serikali.
“Hili la Rais kusafiri sana nalo ni tatizo na wenzetu wameona sisi kama Taifa hatuko makini  na wametumia mwanya huo kutaka kujitenga, kama kuna uongozi imara wasingethubutu kuanza kufanya mambo kama hayo kwa mlango wa nyuma,” anasema Profesa Safari.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Profesa Safari, ni vigumu kwa shirikisho hilo la kisiasa kufanikiwa haraka kutokana na changamoto kadhaa ikiwamo nchi husika kuwa na matatizo ya ndani, hasa ya kidemokrasia ambayo yalitakiwa kupatiwa ufumbuzi kwanza.

No comments:

Post a Comment