aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Monday, August 19, 2013

WAKENYA WAHUSISHWA NA KILIMO CHA BANGI TARIME....


KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, amesema kilimo cha bangi wilayani Tarime kinafadhiliwa na wafanyabiashara wa nchini Kenya. Kamanda Kamugisha aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati alipokuwa akisimamia uteketezwaji wa ekari 16 za bangi. “Bangi inayolimwa Tarime na Rorya inasemekana hufadhiliwa na Wakenya, lakini tutaendelea kupambana ili kutokomeza biashara ya zao hilo,” alisema Kamanda Kamugisha. 
Pamoja na hayo, aliwashutumu baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi pamoja na baadhi ya watumishi wa Serikali, kwamba wanajihusisha na biashara hiyo haramu.

“Kuna maofisa wa polisi wasio waaminifu wanavujisha siri tunapoandaa mkakati wa kutokomeza zao hili katika Wilaya za Tarime na Rorya na hali hii inaonyesha wanahusika moja kwa moja na biashara hii,” alisema.

Alisema operesheni hiyo ni endelevu na akawataka wananchi waungane na Serikali katika kutokomeza zao hilo kwa sababu madhara yake ni makubwa katika jamii.

Wakati wa uteketezaji wa bangi hiyo, vyombo vya dola vilivyohusika ni pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, polisi jamii, mgambo, Idara ya Uhamiaji na wananchi waishio katika Vijiji vya Kemange na Nyagisya, wilayani Tarime.

Miongoni mwa mashamba yaliyoteketezwa ni pamoja na shamba la Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyansurura Mwita Manguri.

No comments:

Post a Comment