aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Thursday, August 15, 2013

UPDATE:PONDA ASOMEWA MASHTAKA MAPYA KITANDANI KISA HATI YA MASHTAKA ALIYOSOMEWA MWANZO IMEJAA KASORO...


KATIBU wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesomewa shitaka la uchochezi, akidaiwa kuhamasisha wafuasi wake kufanya makosa katika maeneo mbalimbali nchini.

Sheikh Ponda alisomewa shitaka hilo jana, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji ya Muhimbili (MOI), mahala alikolazwa akitibiwa jeraha linalodaiwa lilitokana na kupigwa risasi.

Alisomewa shitaka hilo saa 10:20 jioni na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Riwa.

Katika shitaka hilo, Kweka alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kati ya Juni 2 na Agosti 11, mwaka huu, ambapo aliwahamasisha wenzake kufanya vurugu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
 
Kweka alidai kuwa Ponda alitenda kosa hilo katika eneo la Dar es Salaam, Zanzibar na Morogoro, kwa nyakati tofauti.

Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana shitaka lake na kesi yake iliahirishwa hadi Agosti 28, mwaka huu, itakapotajwa kwa ajili ya kusikilizwa.

Mshitakiwa ameendelea kuwa chini ya ulinzi hospitalini hapo baada ya kunyimwa dhamana, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama.


 WAKILI WA PONDA
Wakili wa Ponda, Juma Nassoro, alikosoa hati ya mashitaka aliyosomewa mteja wake, akisema kuwa imejaa kasoro na kueleza kuwa anakusudia kuipinga ili kesi hiyo iweze kufutwa.

Massoro alisema Mahakama ya Kisutu haina haki ya kusikiliza kesi hiyo kutokana na kudai kuwa mteja wake alifanya kosa katika sehemu mbalimbali za Jumhuri ya Muungano ya Tanzania.

“Nimeona kuwa kuna hoja mbili za kuzipinga Agosti 28 kutokana na hati hii kuwa na makosa mbalimbali. “Pia Agosti 11 tayari Ponda alikuwa hospitali chini ya uangalizi wa madaktari, kwa hiyo asingeweza kutenda kosa tena,” alisema.

Wakili huyo alisema anashangazwa na hatua hiyo, kwa maelezo kuwa aliitwa jana kwa ajili ya Sheikh Ponda kuhojiwa saa 8:00 mchana, hivyo alishangaa kuona mteja wake akisomewa mashitaka.

Nassoro alipinga Ponda kuhojiwa, kwani tayari alikuwa amewasilisha barua Tume ya Utawala Bora kupinga tume iliyoundwa ya Jeshi la Polisi kuchunguza tukio la Ponda kupigwa risasi.

“Tuliwasilisha barua hiyo kwa kuwa tayari Jeshi la Polisi lilishatoa msimamo wake kuwa hawakuhusika na tukio la kumpiga risasi Sheikh Ponda.

“Pia leo (jana) haikuwezekana kuhojiwa kwa kuwa tulipinga kutokana na Sheikh kuwa na hali mbaya, kwani ana maumivu ya jeraha, kichwa na kizunguzungu hivyo mahojiano hayakuweza kufanyika,” alisema.

Nassoro alisema baada ya kukaa kwa muda mrefu hakimu hakuweza kufika hadi muda wa kazi ukaisha, lakini cha kushangaza baada ya kuondoka hospitalini hapo hakimu aliwasili.

“Tumekaa muda mrefu hospitali, baadaye tuliamua kuondoka kwa kuwa muda wa kazi ulikuwa umemalizika. Tulipoondoka hakimu akafika na kusoma shitaka, ndipo tulipopigiwa simu kuwa hakimu amekuja,” alisema.

Alisema Ponda ameachwa chini ya ulinzi wa askari kwa kuwa bado ana hali mbaya na anaendelea kupata matibabu kutoka kwa madaktari.


 Mashitaka ya awali
Oktoba 18 mwaka jana, Ponda na wenzake 49 walishitakiwa kwa makosa manne, likiwamo la uchochezi ambapo alihukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja na wenzake kuachiwa huru.

Makosa hayo ni kula njama na kutenda kosa, kuingia kwa nguvu na kujimilikisha kiwanja cha Markaz Chang’ombe, mali ya Kampuni ya Agritanza.

Pia waliweza kujimilikisha kiwanja hicho kwa njia ya uvamizi, iliyopelekea uvunjifu wa amani, wizi, ambapo baada ya kuvamia waliiba vifaa na malighafi, ikiwemo nondo, kokoto zenye jumla ya thamani ya Sh. 59,650,000, mali ya kampuni ya Agritanza.

Kosa la tano ni la uchochezi, ambalo lilimkuta Sheikh Ponda peke yake, ambapo alidaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 12, mwaka jana, katika eneo hilo kwa kuwahamasisha washitakiwa hao watende kosa hilo.


 Madai ya kupigwa risasi
Agosti 10 mwaka huu, Sheikh Ponda Issa Ponda, alijeruhiwa kwa kitu kinachosadikiwa kuwa ni risasi mkoani Morogoro, akihutubia mkutano wa kidini.

Sheikh Ponda alifikishwa MOI Agosti 11 mwaka huu, akiwa tayari amepata tiba ya awali, ambapo uchunguzi wa madaktari wa hospitali hiyo uligundua kuwa mfupa wa bega lake la kulia umevunjika.

Hata hivyo taarifa ya madaktari hao ilisema kuwa wataalamu wameshindwa kugundua jeraha hilo limesababishwa na kitu gani, kutokana na kwamba alikuwa amepata matibabu sehemu nyingin
e.

No comments:

Post a Comment