WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameonja joto baada ya wananchi wa maeneo ya Mloganzira na Kwembe Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kulala barabarani kama njia ya kushikiniza kutekelezewa madai yao. Pinda alikwenda Kwembe kutuliza mgogoro uliotokana na wananchi kudai fidia za viwanja vyao vilivyochukuliwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili (MUHAS), ambapo majengo ya kisasa yanatarajiwa kujengwa katika eneo hilo.
Chuo hicho kinatarajiwa kujengwa mpakani katika eneo hilo la mpakani kati ya Mlogazira (Pwani) na eneo la Kwembe lililopo Wilaya ya Kiondoni Mkoa wa Dar es Salaam.
Mbali na Pinda viongozi wengine waliokumbwa na dhahama hiyo ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ambaye alikuwa ameandamana na maofisa kutoka MUHAS.
Licha ya askari polisi kufanya kazi kubwa ya kutuliza ghasia lakini juhudi hizo ziligonga mwamba kutokana na wananchi hao kuendelea kukaa na wengine kulala barabarani.
Pinda ambaye alifika katika eneo hilo saa saba mchana alikuta viongozi kadhaa waliotangulia katika eneo hilo wamezuiwa na wananchi hao ambao walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alijaribu kuwasihi wakazi hao wapishe viongozi lakini waligoma kuondoka wakipaza sauti za kumtaka waziri mkuu.
Hali hiyo ilimlazimu Pinda kushuka katika gari na kuwahisi wananchi hao waende katika eneo la mkutano ili kuweza kuzungumza kero zao badala ya kulala barabarani.
Kauli hiyo ya Pinda ilionyesha kushusha jazba za wananchi hao ambao waliamua kutii ushauri huo na kwenda katika eneo la mkutano.
Akizungumza katika mkutano huo, mjumbe wa kamati ya madai Frederick Chole, alisema jumla ya wakazi 2,335 walipewa fidia ya awali lakini haikukidhi mahitaji huku watu 93 wakiwa hawajalipwa fedha zao.
“Tuliweza kwenda Ofisi ya waziri ya ardhi na kupewa mchanganuo ambao ulikuwa unaeleza juu ya fidia ya ardhi na mazao yote yalipo juu ya mashamba na nyumba lakini wakati wa malipo tulikwazwa na malipo kiduchu,” alisema Chole.
“Zoezi zima la ulipaji fidia katika eneo hili lilizungukwa na uchakachuaji katika ofisi ya Manispaa ya Kinondoni na MUHAS (Chuo cha Afya Muimbili),” alisema Chole.
Naye Abasi Tamimu, alimtaka waziri mkuu kuangalia suala hilo kwa kina kwani wananchi wa maeneo hayo wamegeuzwa kafara katika mradi huo.
Akijibu hoja hizo waziri mkuu Pinda, alisema kuwa Serikali imesikia kilio chao hivyo itaanza kulipa fidia kwa kuwalipa watu 93 ambao hapo awali walikuwa hawajalipwa.
“Tutawalipa hawa wasiopewa chochote kwanza na nyie mliolipwa Serikali haiwezi kuwafidia mara mbili labda tuangalie utaratibu wakulifanyia kazi ombi lenu hilo la kupewa viwanja hivyo ngoja nikae na watendaji wangu kisha nitawaletea jibu,”alisema Pinda.
Aliongeza kuwa katika hilo serikali itamua kutumia ubinadamu hili kuweza kupunguza matatizo ya wakazi hao na kuhahidi kushughulikia madai ya uchakachuzi wa fedha kwa wale wote wenye vielelezo.
Hata hivyo wananchi hao waliridhishwa na majibu ya waziri mkuu, wakisema kuwa hawana jambo jingine zaidi ya kusibiri utekelezaji wa kauli ya Pinda kwa kuwa ni kiongizi wa juu serikalini.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick.
No comments:
Post a Comment