aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Thursday, August 22, 2013

MBULGARIA ATUHUMIWA KUIBA MILIONI 12.2/= KWENYE ATM


RAIA wa Bulgaria, Todor Peev (38), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka 20 ya wizi wa Sh milioni 12.2 kupitia mashine za kutolea fedha (ATM).
Peev, ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach, alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka hayo na Wakili wa Serikali, Hellen Moshi mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema.
Wakili Moshi alidai kuwa Peev aliiba fedha hizo katika matawi ya Benki za Posta (TPB) na Benki ya Afrika (BoA) yaliyoko katika maeneo tofauti Dar es Salaam.
Alidai kuwa kati ya Julai 28 na Agosti 4 mwaka huu, mshitakiwa aliiba fedha hizo katika matawi ya Manzese, YWCA, Posta Mpya, Samora Avenue, Mikocheni, Mbezi, Kijitonyama, St Joseph, Ubungo Plaza na Africana.
Mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuweka pingamizi la dhamana dhidi ya mshitakiwa huyo.
Wakili Moshi aliiomba Mahakama isitoe dhamana kwa mshitakiwa, kwa kuwa si raia wa Tanzania hivyo anaweza kutoroka. Pia hati ya makazi ya mshitakiwa, bado iko katika uchunguzi, kwa sababu inawezekana aliingia nchini isivyo halali.
Hata hivyo, mawakili wa mshitakiwa, Mathias Kisegu na Allen Mwakyoma, walipinga hoja hizo na kudai kuwa dhamana ni haki ya msingi ya mshitakiwa, kwa mujibu wa Katiba na kisheria kutokuwa raia wa Tanzania, siyo sababu ya kunyimwa dhamana.
Alidai mshitakiwa anaishi nchini kihalali na ana familia ya watoto, aliongeza kuwa wakati mshitakiwa anakamatwa alipigwa na kujeruhiwa jambo lililosababisha afanyiwe upasuaji mdogo na kushonwa nyuzi sita.
Aidha alidai kuhusu kuishi nchini, Idara ya Uhamiaji ilikuwa na nafasi ya kumhoji lakini haikubaini kama anaishi nchini isivyo halali, jambo ambalo linadhihirisha kuwa anaishi nchini kihalali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote Hakimu Lema aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, mwaka huu atakapotoa uamuzi wa dhamana. Mshitakiwa alirudishwa rumande.

No comments:

Post a Comment