SAKATA la Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, limeendelea kuwa gumzo katika maeneo mbalimbali, huku matamko makali yakitolewa dhidi ya Serikali.
Sakata hilo limeonekana kutikisa na kutawala vyombo vya habari, baada ya kiongozi huyo wa dini kudaiwa kupigwa risasi, kusomewa mashtaka kitandani na baadaye kupelekwa gerezani chini ya ulinzi mkali akitolewa katika Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI).
Suala hilo limeibua hisia nyingine baada ya masheikh jijini Dar es Salaam, kutoa tamko lenye mwelekeo wa kupinga udhalilishwaji wa kiongozi huyo na kuionya Serikali juu ya mwenendo huo.
Mbali na masheikh kutoa tamko jana, Jeshi la Polisi kwa upande wake nalo liliimarisha ulinzi katika Msikiti wa Kichangani, uliopo Magomeni na ule wa Mtambani uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba, alisema kitendo hicho ni kibaya kwani kinapandikiza chuki baina ya Waislamu na Serikali.
Sheikh Katimba ambaye alikuwa ameongozana na masheikh kadhaa akiwamo Amiri wa Shura ya Maimamu, Sheikh Musa Kundecha, alitoa tamko hilo katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana.
“Tunalaani kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda, tukio la kupigwa risasi na baadaye kudhalilishwa kwa kuondolewa hospitali wakati akipatiwa matibabu, ni jambo baya linakwenda kinyume na haki za binadamu.
“Tukio hili limeibua hisia kali kwa Waislamu, hivyo tunaitaka Serikali kuacha kuwatesa na kuwadhalilisha viongozi wa dini ya kiislamu, kwani kufanya hivyo ni kupandikiza chuki miongoni mwa Waislamu.
“Waislamu wamekuwa wakiamini kwamba, ufumbuzi wa suala la amani ya kweli na ya kudumu ya nchi ni kuweza kushughulikia madai ya msingi ya Waislamu dhidi ya Serikali ambayo ndio chanzo cha madai ya kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda,” alisema Sheikh Katimba wakati akisoma tamko hilo lililosainiwa na Sheikh Juma Said Ally.
Waitisha mkutano wa dharura kesho
Kutokana na suala hilo, jumuiya hiyo imeitisha mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho katika viwanja vya Nurul Yakin vilivyopo Wilaya Temeke, jijini Dar es Salaam ambapo tamko litatolewa juu ya mustakabali wa suala hilo.
Katika tamko hilo, Sheikh Katimba alisema kuwa hatua hiyo inaweza kuzidisha chuki baina ya Waislamu na vyombo vya dola kwa madai kuwa vimekuwa vikiwakandamiza Waislamu.
“Kitendo cha kumpiga risasi Sheikh Ponda na kisha kumchukua kutoka hospitali na kumpeleka gerezani kwa kukiuka taratibu ni kinyume cha haki za binadamu.
“Matibabu ni haki mojawapo kwa binadamu yeyote hata kama kuna wanaomtuhumu. Tuhuma si sababu ya kukiuka taratibu, kuvunja sheria na hata kumtisha unayemtuhumu, kwani njia hiyo haiwezi kutatua bali inazidisha ukubwa wa tatizo.
“Tunalaani kwa mara nyingine kitendo cha Polisi na Usalama wa Taifa kutenda vitendo vinavyoashiria uonevu kwa viongozi wa dini ya Kiislamu, pia tunaitaka Serikali kutenda uadilifu kwa raia wake hata pale inapoamini kuwa raia hao wana makosa.
Sheikh Basaleh aonya
Kwa upande wake mjumbe wa Taasisi ya Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Alli Basaleh alikemea vikali tukio la kupigwa kwa Sheikh Ponda na kusema kuwa jamii inapaswa kupinga vitendo vya watu kuteswa na kunyanyaswa vinavyofanywa na vyombo vya dola.
“Hii ni ishara ya huko tuendako kwa baadaye, nchi inaweza kuingia kwenye machafuko, ni wazi kabisa hata katika mataifa ambayo amani imevurugika hali ilianza kama hivi kama njia ya kupinga uonevu wa Serikali dhidi ya watu wake.
“Tuwe makini na hali hii hakuna taifa lolote linaloweza kuhubiri amani pasipo kuwa na umoja na masikilizano baina ya viongozi wa Serikali na watu wake,” alisema Sheikh Basaleh.
Polisi waranda misikitini
Hata hivyo wakati viongozi hao wakiendelea na mkutano na waandishi wa habari jana, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika Msikiti wa Mtambani ambapo gari tatu zilikuwa zikiranda nje ya msikiti huo huku zikiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
MTANZANIA iliwashuhudia askari hao wakiwa katika gari aina ya Defender zenye namba za usajili PT 2118 na PT 2083, ambazo zilikuwa nje ya msikiti huo.
Hata hivyo wakati askari wakiwa wanaranda katika eneo hilo la Msikiti, baadhi ya makundi ya Waislamu walikuwa wakigawa vipeperushi vilivyokuwa vimeandaliwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ambavyo vilihoji. “Kwa nini Serikali ya CCM imempiga risasi Sheikh Ponda?”
Mbali na Msikiti wa Mtambani, askari pia walikuwa wametanda katika Msikiti wa Magomeni Kichangani, ambapo anatoka Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Kundecha.
MTANZANIA ilifanikiwa kunasa kipeperushi kilichosomeka kwa maneno yafuatayo; “Kwa nini Serikali ya CCM imempiga risasi Sheikh Ponda, polisi waliotaka kumuua sasa wamemteka kutoka Muhimbili hadi Segerea akiwa bado mgonjwa.
“Hii imefanyika ili mfumo wa kuwakandamiza Waislamu na kuwapendelea Wakristo uweze kudumu na kuweza kupewa fedha na Serikali chini ya Mkataba (MoU),” ilisomeka sehemu ya kipeperushi hicho.
Alipopigwa mkoani Morogoro
Agosti 10, mwaka huu akiwa mkoani Morogoro, Sheikh Ponda, alidaiwa kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni risasi, ambapo Agosti 15, mwaka huu Jeshi la Polisi nchini liliripoti kushikiliwa kwa askari anayedaiwa kufyatua risasi hiyo.
Katika mahojiano aliyofanya na Gazeti la MTANZANIA Agosti 11, mwaka huu, Sheikh Ponda alisema polisi walidhamiria kumuua kwa makusudi ili wapoteze ushahidi. Huku akidai kuwa jeraha lake analodai limetokana na kupigwa risasi.
Sheikh Ponda alieleza kuwa alipigwa risasi na polisi wakati akiwa kwenye gari na wenzake. “ Nilimuona kwa macho yangu askari mmoja ambaye alikua amevaa sare akinilenga kwa mtutu wa bunduki,” alisema Ponda.
-MTANZANIA
No comments:
Post a Comment