aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Sunday, August 25, 2013

CCM KIKAANGONI



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara nyingine kinapita katika wakati mgumu unaokilazimisha kuchukua maamuzi mazito yatakayonusuru mpasuko na pengine kuendeleza mfumo wa sasa wa muungano wa serikali mbili uliokiasisi.

Mjini Dodoma, ambako vikao vya juu vya maamuzi vya chama hicho vinaendelea, chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, inaripotiwa kuwa ajenda zinazochukua nafasi kubwa ni mjadala wa muundo wa Muungano na vita ya kimakundi ndani ya chama hicho.

Tofauti na ilivyopata kuwa katika vikao vya siku zilizopita, ajenda moja inayoonekana kuleta sura ya mtanzuko ni ile ya mgogoro na mvutano wa kisiasa unaokitafuna chama hicho mkoani Kagera.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu iliyokutana juzi na jana, zinaeleza kwamba hoja hiyo ndiyo ambayo wakati fulani ilikaribia kabisa kusababisha kuchukuliwa kwa hatua za kuadhibiwa kwa vigogo wa chama hicho, ambao majina yao yanatajwa kuwa kiini cha mpasuko huo.

Hali hiyo ilisababisha kupitishwa kwa azimio la kutoa notisi ya wito wa dharura kwa Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagesheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Aman, wanasiasa wanaotajwa kuwa mahasimu wakubwa waliokifikisha chama chao katika hatua ngumu ya sasa.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, uamuzi wa kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa, ikiwa ni pamoja na kupewa onyo kwa viongozi hao wawili na wenzao wengine, ulikuja baada ya hoja iliyotolewa na Rais Kikwete ya kuwataka wazuiwe kugombea nafasi za uongozi mwaka 2015 kubatilishwa.

Mbali na Kagasheki na Amani, viongozi wengine wawili ambao wameitwa Dodoma kwa ajili hiyo hiyo, ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera na Katibu wake.

Sambamba na hilo, kamati kuu hiyo katika kikao chake hicho, ilibatilisha uamuzi wa CCM Mkoa wa Kagera wa kuwatimua na kuwapokonya uanachama madiwani wake wanane.

Wakati Kamati Kuu ikikuna vichwa kusaka amani huko Bukoba, hoja ya pili iliyoonekana kugusa mjadala katika kikao hicho ni ile inayomgusa kada wa siku nyingi katika visiwa vya Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid.

Mansoor, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, waziri wa zamani na mtu aliyepata kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, ameibua mjadala baada ya kuibua hoja ya kutaka Zanzibar kupata haki ya kuwa na mamlaka zaidi ya kujiamulia mambo yake ndani ya Muungano.

Mwanasiasa huyo, ambaye amepata kuwa Mweka Hazina wa CCM Zanzibar wakati wote wa uongozi wa Rais Mstaafu, Amani Karume, amekuwa mtetezi mkubwa wa muundo wa Muungano wa serikali tatu badala ya ule wa sasa wa serikali mbili.

Halmashauri Kuu inatarajiwa kutoa uamuzi wa ama kufukuzwa au kubaki kundini kwa Mansoor, ambaye uongozi wa ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na kamati maalumu ya CCM Zanzibar, vilipendekeza atimuliwe kutokana na msimamo wake huo.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwa waandishi wa habari ilieleza kuwa CC imejadili kwa kina muundo wa Muungano na suala la Mansoor, ambaye amekwishatangaza kuwa yuko tayari kufukuzwa kwa sababu ya kutofautiana na chama chake kuhusu muundo wa sasa wa Muungano.

Nape alisema, hatima ya Mansoor imeachwa mikononi mwa NEC, baada ya Kamati Kuu kupokea mapendekezo ya vikao vya chama hicho katika ngazi za wilaya, mkoa na Kamati Maalum ya CCM Zanzibar, kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

“Kamati Kuu imejadili suala la Mansoor, hasa baada ya kupokea mapendekezo yote kuanzia ngazi za chini, yaani vikao vya wilaya, mkoa pamoja na kile cha kamati maalum ya CCM Zanzibar na tumetoka na uamuzi wa pamoja ambao hatima yake itafikishwa mbele ya NEC,” alisema Nape.

Sakata la muundo wa Muungano ambalo liliibuka kwa nguvu wakati wa mjadala wa muundo wa Katiba Mpya limewagawa wana CCM Zanzibar katika makundi matatu, yakiwemo yale yanayotaka muundo wa sasa wa serikali mbili, serikali moja pamoja na lile linalopigia chapuo muundo wa serikali ya mkataba.

Katikati ya sakata hili, kuibuka kwa Mansoor na kueleza msimamo wake, huku akitangaza kuwa tayari kufukuzwa kwa kuutetea msimamo wake, kunaiweka hatarini sera ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, inayoamini katika muundo wa serikali mbili.

Taarifa kutoka Dodoma zinaeleza kuwa, iwapo NEC itabariki uamuzi wa Kamati Kuu wa kumvua uanachama Mansoor, itakuwa ni turufu muhimu kwa Chama cha Wananchi (CUF) kujiimarisha kisiasa na pia mpasuko ndani ya chama kutokana na kuwepo baadhi ya viongozi wastaafu wa CCM wanaodaiwa kuwa nyuma yake.

Wakati hayo yakijiri, kwa upande mwingine mgogoro baina ya Balozi Kagasheki na Meya Amani iwapo hautapatiwa ufumbuzi wa kudumu katika vikao vya sasa, unaweza kuwa mwanzo wa kuchipuka upya kwa upinzani na anguko la CCM katika siasa za ushindani mkoani Kagera.

Zipo taarifa zinazoeleza kuwa, tayari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekwishajipanga kuwapokea madiwani wanane ambao uongozi wa mkoa ulipitisha uamuzi wa kuwafukuza, kwa madai ya kukivuruga chama hicho.

Ajenda ya mgogoro wa Kagasheki na Amani ililazimika kufikishwa katika vikao vya CC na Halmashauri Kuu, baada ya kusitishwa kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera wa kuwavua uanachama madiwani wanane, kwa madai ya usaliti na kuungana na wenzao wa upinzani, wakitaka kumng’oa Meya Amani.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu zinaeleza kuwa, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, alitoa nafasi kubwa ya kujadiliwa kwa mgogoro huo ambapo wajumbe walipendekeza wote wawili, Kagasheki na Amani, wasiruhusiwe kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza kuwa Rais Kikwete alilazimika kuhitimisha mjadala huo kwa kuwataka wajumbe kutambua kuwa iwapo chama hakitakuwa makini na viongozi hao wawili, kuna hatari ya CCM Mkoa wa Kagera kupasuka na kukosa ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wakati huo huo, taarifa nyingine kutoka mjini Dodoma zinaeleza kuwa, Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, jana aliwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya makatibu wa mikoa na wilaya wa nchi nzima, kwa ajili ya kupata baraka za Halmashauri Kuu kabla ya kutekelezwa.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa mabadiliko hayo yanalenga kukiwezesha chama hicho kujiimarisha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, kwa kuwaondoa watendaji wake wote wanaoonekana kupwaya na kuingiza sura mpya zenye uwezo wa kuhimili mtikisiko wa sasa wa kisiasa.

Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Kikwete alizindua Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, ambalo Mwenyekiti wake ni Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Katibu wake ni Spika mstaafu wa Bunge, ambaye amepata pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa.

Wajumbe wengine wanaounda baraza hilo ni Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na marais wastaafu wa Zanzibar, Salmin Amour na Amani Abeid Karume.

Mwingine atakayejumuika katika baraza hilo ni Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Bara, John Samuel Malecela.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa baraza hilo, Kikwete alisema limeundwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Ibara ya 127 na litakuwa na kazi ya kushauri pale litakapoona inafaa.

No comments:

Post a Comment