aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Sunday, August 25, 2013

WAZIRI KAGASHEKI APIGWA STOP KAFANYA SIASA HADI MWAKA 2015

napekagasheki_60ad9.jpg
Dodoma. Suala la kutimuliwa kwa madiwani wanane wa CCM katika Manispaa ya Bukoba limeingia sura mpya baada ya Kamati Kuu kuwazuia Meya, Dk Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kushiriki katika siasa mkoani humo hadi mwaka 2015. P.T

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika mgogoro wa viongozi hao, unakiumiza chama katika jimbo hilo.
Taarifa zilidai chanzo cha ugomvi kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani, ni kwa kila mmoja kutaka kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Bukoba mjini katika uchaguzi ujao. Na kwa uamuzi huo, Kagasheki na Dk Amani hawatashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo, akitangaza uamuzi huo jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, 
Nape Nnauye alisema viongozi hao watakutana na Kamati Kuu leo na baada ya hapo utatangazwa uamuzi uliofikiwa.
Mbali na meya na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, wengine walioitwa katika kikao hicho cha leo ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Costansia Buhinye, katibu wake, Averin Mushi pamoja na mwenyekiti wa chama Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na katibu wake, Janath Kayanda.
Kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu ambayo ilimaliza kikao chake saa 8:30 usiku wa kuamkia jana italazimika kukaa tena leo kuwaelezea uamuzi uliofikia.
Kumekuwapo na mgogoro mkubwa katika Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, ukimuhusisha Kagasheki na baadhi ya madiwani kwa upande mmoja; na Dk Amani na kundi jingine la madiwani kwa upande mwingine.
Wakati wa mgogoro huo madiwani wamekuwa wakituhumiana ufisadi, na CCM imekwishawatuma viongozi wake wa juu kuingilia kati mgogoro huo akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana.
Kufikishwa kwenye Kamati Kuu kwa suala hilo kumekuja baada ya uongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kuamua kuwatimua uanachama madiwani hao, hatua ambayo ilikuwa inahatarisha nafasi zao na hivyo kukiingiza chama hicho kwenye uchaguzi mdogo.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi hao kuwajibishwa kwa kukiuka kanuni, kwa kuwa upo uamuzi wa chama unaokataza viongozi waliochaguliwa katika vyombo vya dola kuwajibishwa kwa staili hiyo.
Madiwani waliovuliwa uanachama na kata zao katika mabano ni pamoja na Richard Gaspar (Miembeni ), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai).
Wengine ni Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Baada ya kutimuliwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema chama Mkoa wa Kagera hawana uwezo wa kuvua uanachama na kwamba wenye uwezo huo ni ngazi ya taifa.
Nape alisema kwa mujibu wa taratibu za CCM, Mkoa wa Kagera walitakiwa kuwasilisha tuhuma hizo ngazi za juu ili zijadiliwe na kuamuliwa na Kamati Kuu (CC).
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu, viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kama wabunge na madiwani, hawawezi kuvuliwa uanachama na vikao vya chini bali chombo chenye mamlaka hayo ni Kamati Kuu.
Hata hivyo, siku moja baada ya tamko hilo la Nape, CCM mkoani Kagera kilisisitiza kuwa uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao ni halali, kwa kuwa ulifanywa na kikao halali kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye, alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, hakuna kikao chochote ndani ya chama kinachoweza kukinzana na kikao kingine kwa hivyo, bado madiwani hao wamefutiwa dhamana ya uanachama kama mkoa ulivyoamua.
Buhiye alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa ndicho kikao kikuu chenye uamuzi wa kumwajibisha mwanachama yeyote, iwapo atabainika kwenda kinyume cha taratibu na kanuni za chama, kwa mujibu wa katiba ya CCM.
Suala la Mansour
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imelipeleka suala la kutimuliwa uanachama kwa Mwakilishi wa Kiembesamaki Zanzibar, Mansour Yusuf Himid kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambako litajadiliwa leo na kutolewa uamuzi.
Nape alisema mamlaka ya mwisho ya kumteua mwakilishi ni NEC, hivyo lisingeweza kujadiliwa na Kamati Kuu.

No comments:

Post a Comment