Watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino) wamewalalamikia wazazi wao kwa kuwatelekeza katika vituo wanavyolelewa baada ya kupelekwa huko kwa ajili ya usalama wao.
Watoto hao wametoa malalamiko yao kupitia risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, katika kilele cha Summer Camp waliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Under the Same Sun.
Severine Edward ambaye aliwakilisha wenzake, alisema kuwa kutoka kipindi chwa mwaka 2010 yalipozuka mauaji ya albino na kupelekwa katika vituo kwa ajili ya ulinzi, wazazi wao wamewasahau na wamekuwa wakiishi kama yatima.
“Tumekuwa kama yatima tunakumbukwa zaidi na watu baki kuliko wazazi wetu waliotuleta dunia kweli tunaumia sana na matendo yao” alisema Edward.
Katika risala hiyo, aliiomba Serikali kujitokeza na kuwasaidia misaada mbalimbali kama kuwapatia madaktari kwa sababu hilo limekuwa ni changamoto kutokana na hali ya ngozi zao.
Alisema kuwa wanaishukuru shirika la Under the Same Sun kwa kuwa walezi wao wakubwa katika huduma zote ikiwamo elimu ambapo wamewaweka katika shule ambazo ni salama kwao.
Hata hivyo, mgeni rasmi alisema kitendo kinachofanywa na wazazi pamoja na walezi kuwatelekeza watoto wao kwa sababu kuna wafadhili siyo cha kibinadamu na kuwataka kuwa karibu na watoto ili waweze kupata malezi bora.
Watoto na watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakikumbwa na adha kubwa ya kuuawa na kisha kukatwa baadhi ya viungo vya miili yao na baadhi ya watu wenye imani potofu kuwa viungo hivyo vinawawezesha kupata, mafanikio hususan katika biashara zao.
Mkoa wa Mwanza ni moja ya mikoa iliyokumbwa na mauaji ya albino ambao katika kipindi cha mwaka huu jumla ya albino wanne walivamiwa na kukatwa viungo sehemu mbalimbali za mwili wao, huku mmoja kati ya hao kufariki dunia.
No comments:
Post a Comment