aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Wednesday, August 14, 2013

WALIORUDI RWANDA WAANDALIWA ARDHI....


                     Rais Paul Kagame wa Rwanda
  
WAKATI agizo la Rais Jakaya Kikwete la wakimbizi haramu likiendelea kutekelezwa na kupokewa vizuri na Rwanda, Bodi ya Kilimo ya nchi hiyo (Rab) imetenga zaidi ya hekta 300 za ardhi kwa ajili ya wananchi wanaorejea.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, ambaye ni Kaimu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Elizeus Mushongi, alisema hadi jana, wahamiaji haramu 7,814 walikuwa wameondoka mkoani Kagera na ni walioripoti katika vituo vya Uhamiaji mkoani hapa.
Mushongi alisema idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na wahamiaji wanaoondoka kupitia ‘njia za panya’ ambao ni wengi zaidi.
Alisema katika makundi hayo ya wahamiaji haramu, ambao wanatoka Uganda, Burundi na Rwanda kuna wengine ambao hawataki kurudi kwao na idadi kubwa ya wasiotaka kurudi ni Wanyarwanda.
Kwa mujibu wa Mushongi, Wanyarwanda hao wakati wakijiorodhesha katika vituo, wamekuwa wakisema wanakwenda Burundi na Uganda na hata walioonekana kupita ‘njia za panya’, walikuwa wakienda nchi hizo pia.
Alisema katika kituo vya Murusagamba, walipita Wanyarwanda 35 wakienda Burundi, kituo cha Mutukula, Wanyarwanda 13 wakielekea Uganda, Bugango 22 wakienda Uganda na Kanyigo saba, wakienda Uganda.
Katika kituo cha Kabanga, Warundi 522 walijisajili kurudi kwao na Warundi 10 katika kituo cha Murongo, walisema wanakwenda Uganda. Katika kituo hicho, Wanyarwanda 166 walipita wakienda Uganda.
Rusumo yaongoza
Aliongeza kuwa kituo cha Rusumo kinaongoza kwa kupitisha wahamiaji haramu wengi, waliofikia 4,748 wakienda Rwanda.Kituo cha Murongo kilipitisha wahamiaji 332, Murusagamba 78 na Mutukula 31 na eneo la Mgoma ambalo halina vituo vya Uhamiaji, walijisalimisha 1,734 katika ofisi za vijiji.
Kuhusu silaha zilizosalimishwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, alisema silaha 42 zilisalimishwa na wahamiaji hao.
Alisema miongoni mwa silaha hizo, nyingi ni magobori huku akisema Jeshi lake limejipanga kukabiliana na wahamiaji ambao hawajaondoka. Alisisitiza kuwa wahamiaji watakaokamatwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Rwanda yakataa ng’ombe
Mushongi aliendelea kusema idadi ya ng’ombe walioondoka hadi jana ni 1,996 kupitia kituo cha Rusumo huku wengi wakienda Uganda, kwa sababu Rwanda haitaki idadi kubwa ya ng’ombe.
Kitakwimu, alisema kati ya wahamiaji haramu walioondoka kwa hiyari, Wanyarwanda ni asilimia 64, Warundi asilimia 34 na Waganda, asilimia mbili. Alisema msako maalumu haujaanza, lakini unatarajiwa kuanza muda wowote na maandalizi yamekamilika.
Hata hivyo, alitaka wahamiaji hao haramu waendelee kuondoka kwa hiari yao kabla hawajafikishwa kwenye mkono wa sheria. Alisema Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kagera, imesitisha utoaji vibali kwa muda wakisubiri maelekezo kutoka juu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe aliwahadharisha wananchi kuwa makini wakati wa msako wa wahamiaji haramu, na kufichua waliojificha.Alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria watakaobainika kuficha na kuwakingia kifua wahamiaji hao.
Ardhi iliyotengwa
Ardhi hiyo imetengwa katika wilaya za Nyagatare na Gatsibo kwa ajili ya wafugaji ili mifugo yao ipate malisho, imefahamika. Takribani mifugo 2,000 kwa mujibu wa gazeti la The New Times la Rwanda, wameingia nchini humo kutoka Tanzania tangu Wanyarwanda ambao ni wahamiaji haramu, watekeleze agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuondoka katika mapori mkoani Kagera na kurudi kwao.
Baada ya agizo hilo kutekelezwa, wafugaji na wakulima hao walionesha wasiwasi wao wa kupata maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.
Hata hivyo, Mratibu wa Rab katika Jimbo la Mashariki, Celestin Nyambyi, alisema juzi kuwa mifugo hao watawekwa katika vituo maalumu vyenye karantini kwa hadhari ya usalama.
“Ng’ombe wanaingia nchini kwa idadi kubwa na hivyo kuwapo uwezekano wa kusababisha tishio la kiafya kama hadhari haitachukuliwa … wafugaji wanaorejea watapata mahitaji yote wanayotaka kwa ajili ya kupata makazi ya kudumu nchini mwao,” alisema Nyambyi.
Zaidi ya Wanyarwanda 3,500 wanaoishi katika wilaya za Biharamulo, Ngara, Karagwe na Muleba tangu miaka ya sitini hadi sasa, wamepokewa baada ya kufukuzwa Tanzania, gazeti hilo liliripoti.
Wakizungumza na gazeti hilo juzi, wafugaji hao walilalamikia walichokiita kutendwa vibaya na mamlaka za Tanzania na wenyeji, wakidai kuwa walifukuzwa nchini bila kuzingatia haki za msingi za kibinadamu.
Alex Rurangwa, mfugaji ambaye familia yake ilikuwa na ng’ombe 3,000 wilayani Biharamulo, alisema walinyanyaswa na hawakuruhusiwa kuondoka na ng’ombe hao.
Alishauri Wanyarwanda wengine walioko Tanzania kuondoka kabla hawajapata hasara ya mali na maisha.
“Wanyarwanda wote wanapaswa kuondoka Tanzania. Kuna mazingira yamewekwa ambayo yanaruhusu wakulima kupoteza mali nyingi. Mazingira ya kila mmoja kupora mali za Wanyarwanda ndiyo yameandaliwa,” alidai Rurangwa.
“Wana kila haki ya kutufukuza kutoka nchini mwao, lakini si watupige risasi na kutuibia ng’ombe kama walivyofanya. Nilipoteza ng’ombe 30 kwa kundi lisilojulikana la watu. Walimvizia kaka yangu na kumjeruhi,”alidai.
Mmoja wa wakimbizi waliorejea, Ben Celestin (26), alikuwa akipata matibabu katika hospitali ya Kirehe juzi baada ya kudai kupigwa mshale mgongoni.
Rurangwa alisema ng’ombe waliorudi nao ndio walikuwa chanzo pekee cha mapato yao, ingawa wanataka kuwabadilisha kwa chanzo kingine cha uzalishaji mali.
“Tumepata hasara kubwa; tunahitaji sasa kubadilisha shughuli ambayo tumekuwa tukiifanya kwa muda mrefu. Tutauza wengi ili kununulia ardhi, nyumba na kuishi maisha ya kudumu. Tunaomba wauzaji wengine waturuhusu tuuze wa kwetu kwanza, kama dharura.”
John Mugisha, mkulima ambaye ng’ombe wake bado wako njiani kutoka wilayani Karagwe, alikuwa na wasiwasi kama wote watafika nchini humo. Alisema vizuizi vya asili kama milima, mito na hifadhi za wanyamapori kwamba vinaweza kuzuia safari ya ng’ombe hao.
“Tuna matatizo. Siku tulizopewa (14) na tulivyotendwa ni ukiukwaji wa haki zetu. Karagwe ni mbali sana na Rwanda. Ng’ombe wetu wako njiani wakijaribu kuvuka mito na mabwawa. Hivyo, nina shaka kama watafika hapa kwa wakati mwafaka,” alisema.
Mume Mtanzania
Roda Mungeriwase (42), mama wa watoto wanane, alidai kuwa kuishi Tanzania siku zote kumekuwa kwa matatizo kwa Wanyarwanda.
“Nililazimika kumwacha baba wa watoto wangu saba ili atunze mali zetu. Mume wangu ni Mtanzania. Wazazi wangu waliingia Tanzania mwaka 1966. Maisha haya ya mashaka yamekuwa sehemu ya maisha yetu,” Mungeriwase alidai.
“Ni hali ya kutisha pale ambapo kwa ghafla tu mtu anajikuta hana mali na nyumba, familia zimesambaratika. Sijui majaaliwa ya mume wangu au jinsi atakavyolea watoto wetu hao saba,” alilalamika.
Mapema, iliripotiwa kuwa makataa waliyopewa Wanyarwanda kuondoka Tanzania yalikuwa Agosti 9. Hata hivyo, kwa mujibu wa wakimbizi waliorejea, Wanyarwanda wote waliokuwa wakituhumiwa kuishi nchini Tanzania kiharamu walitakiwa hadi leo wawe wameondoka nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Gazeti hilo hakuna mahali limezungumzia jinsi Wanyarwanda hao walivyoingia nchini kama walifuata taratibu au walikuwa haramu.

No comments:

Post a Comment