NYUMBA sita katika eneo la Mbwewe wilayani Bagamoyo mkoani Pwani zimeteketezwa kwa moto na watu. Inaelezwa kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya kudaiwa kuwa wakazi wa nyumba hizo walihusika na wizi wa marobota na viatu yaliyokuwamo katika gari ya Fuso iliyopata ajali katika eneo hilo.
Gari hiyo ilipata ajali katika eneo la Mbwewe katika barabara ya Chalinze- Segera baada ya gurudumu la nyuma upande wa kushoto kupasuka na kusababisha ipoteza muelekeo na kuziba njia kwa saa kadhaa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulirch Matei, alisema gari hilo lilikiwa likiendeshwa na Zakayo Joseph akiwa na watu wengine wawili.
Alisema baada ya kupinduka wakazi wa eneo hilo waliiba marobota na viatu vilivyokuwamo na kutokomea navyo majumbani kwako.
Matei alisema dereva Joseph na wenzake wawili walifanya msako kwa kushirikiana na wasamaria wema kwa kupita nyumba hadi nyumba na ndipo walibaini kuwa marobota hayo yaliibwa katika nyumba hizo.
Alisema wenye nyumba hizo walipigwa na kuchomewa moto nyumba zao.
Watu waliopigwa na kuchomewa moto nyumba zao ni Athumani Seif, Togeza Motua, Mwajuma Adam, Mustafa Rajab, Shabani Rajab, Said Khalfan na Zuhura Adam ambao walikimbizwa katika Kituo cha Afya Mwewe kupatiwa matibabu.
Matei alisema uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea na amewaasa wananchi kuachana na tabia ya kuiba inapotokea ajali.
No comments:
Post a Comment