George Mwakajinga
Vikongwe wawili wakazi wa Kata za Rutamba na Mingoyo mkoani Lindi, wameuawa kwa kushambuliwa kwa silaha mbalimbali, ikiwamo jembe na mapanga kwa madai ya imani za kishirikina.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, George Mwakajinga, vikongwe haowaliuawa Julai 29 na 30 mwaka huu, saa 9:30 na 10:30 alasiri.
Mwakajinga amewataja marehemu hao kuwa ni, Esha Mohamedi (81) mkulima wa kijiji cha Kinyope, Kata ya Rutamba, Lindi Vijijini na Mary Albert (61) wa kata ya Mingoyo, Manispaa ya Lindi.
Amefafanua kuwa Esha aliuwawa kwa kukatwa na jembe shingoni na mtu aliyemtaja kuwa ni Said Kanduti (31), Jumatatu iliyopita wakati akienda porini kutafuta kuni.
Mwakajinga akasema Esha kabla ya umauti kumkuta alimuaga mume wake kuwa anakwenda porini kutafuta kuni na kwamba akiwa njiani ndipo alikutana na Kanduti ambaye alimkata shingoni na kufariki dunia.
Kamanda Mwakajinga alisema baada ya Esha kufariki dunia, mtuhumiwa huyo aliuchimbia chini mwili wa marehemu huku akikata baadhi ya viungo kama sehemu za siri na kuondoka nazo.
Alisema baada mume wake kutomwona mke wake alitoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji ambayo iliitisha kikao kwa ajili ya kumtafuta ndipo wanakijiji walifanikiwa kuugundua ukiwa umechimbiwa chini pembezoni mwa shamba la mtuhumiwa.
“Katika msako huo, akiwamo na mtuhumiwa mwenyewe walifanikiwa kuukuta mwili huo umefukiwa chini, huku akiwa na majeraha shingoni, ndipo wananchi wakambana Kanduti na kukosa jibu na kumweka chini ya ulinzi na kumfikisha Polisi,” alisema.
Mwakajinga alisema mtuhumiwa amekiri kumuua Esha huku akieleza alidanganywa na mmoja wa waganga wa kienyeji kupata baadhi ya viungo vya mwili wa mtu mzima kushughulikia shamba lake ili apate mazao mengi.
Katika tukio la pili, Mwakajinga alisema Mary Albert aliuawa Julai 30 mwaka huu, saa 9:30 mchana kijiji cha Ruhokwe kwa kukatwa mapanga kichwani na mtu aitwaye Hassani Hamisi maarufu kama Vasco.
Alisema Mary alikwenda Ruhokwe kusalimia ndugu zake ndipo Vasco alifika nyumbani hapo na kumshambulia kwa kumkata mapanga kichwani na kufariki dunia.
Alisema baada ya tukio hilo mtuhumiwa huyo alikimbia na Jeshi hilo linaendelea kumsaka ili sheria ichukue mkondo wake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment