KATIBU wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, amesomewa shitaka la kuwahamasisha wafuasi wake kutenda makosa.
Ponda (54), alisomewa shitaka hilo jana katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (MOI), alikolazwa akitibiwa jeraha analodai ni la risasi, lililoko bega la kulia.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Riwa, alimsomea shitaka hilo saa 10.15 jioni.
Kweka alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Juni 2 na Agosti 11, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali nchini.
Alidai kwa wadhifa wake, Ponda aliwahamasisha wafuasi wake kufanya vurugu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Ponda alikana shitaka na kesi iliahirishwa hadi Agosti 28, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.
Mshitakiwa ameendelea kuwa chini ya ulinzi hospitali hapo, baada ya kunyimwa dhamana kutokana na sababu za kiusalama.
Kwa upande wake, wakili Juma Nassor, anayemwakilisha Ponda, hakuwepo wakati shitaka hilo likisomwa.
Hata hiyo, ilielezwa wanatarajia kuwasilisha pingamizi mahakamani kutaka kesi hiyo ifutwe wakidai hati ya mashitaka ina kasoro kisheria.
Miongoni mwa kasoro hizo inadaiwa ni kufunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambayo haina uwezo wa kusikiliza shitaka hilo linalodaiwa kutendwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Licha ya kuwepo ulinzi mkali katika maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wafuasi wa Ponda walifurika na kusababisha usumbufu kwa watu wengine, wakiwemo waliokwenda kupata huduma ya tiba na kuona wagonjwa.
Mmoja wa madaktari katika hospitali hiyo kubwa nchini, ambaye hakutaka kutaja jina, alikaririwa akisema ni vyema Ponda akahamishiwa hospitali nyingine ili kupunguza msongamano usio wa lazima Muhimbili.
Alisema jeraha la Ponda linaweza kuendelea kutibiwa katika hospitali zingine zilizoko jijini Dar es Salaam na si lazima Muhimbili.
Ponda alipokewa MOI Agosti 11, mwaka huu, saa 7.30 mchana, akitokea MNH.
Inadaiwa kiongozi huyo alijeruhiwa mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa mkoani Morogoro, baada ya kumaliza kuhutubia kongamano la baraza la Idd el Fitri, lililoandaliwa na taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment