aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Monday, August 26, 2013

KISENA:TUKO TAYARI KUNUNUA HISA ZOTE ZA UDA....


KAMPUNI ya Simon Group ambayo ni mwekezaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) imesema iko tayari kununua hisa zote za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikiwa hatojitokeza mnunuzi mwingine. Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya halmashauri hiyo kutangaza kujitoa katika usimamizi na uendeshaji wa UDA kwa kuuza hisa zake zenye thamani ya Sh milioni 3.63 sawa na asilimia 51. 
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena, alisema taarifa za jiji kujitoa hazijamfikia rasimi bali amezisikia kupitia vyombo vya habari.

“Nimesikia jiji wamejitoa na wanauza hisa zao, Simon Group tuko tayari kununua hisa hizo, kama atatokea Mtanzania mwingine anataka kununua hatuna tatizo.

“Kumekuwapo na maneno mengi kuwa Simon Group ni mafisadi, tunaeleza wazi kuwa sisi si mafisadi hatunyang’anyi mali za UDA.

“Ni wawekezaji wazalendo tunawekeza kwa maslahi ya umma bila kubagua,” alisema Kisena.

Akizungumzia suala la madai yaliyopo mahakamani ya kesi mbalimbali yanayolihusu UDA yenye thamani ya Sh bilioni 17 ambayo Jiji limedai ni moja ya sababu ya kujitoa alisema hawana tatizo na ikifika wakati wa kununua watanunua na madeni yote.

Alisema hayuko tayari kuzungumzia suala la kulipia hisa zilizogawiwa alizoingia mkataba wa awali na Bodi ya UDA kwa sababu Jiji halijampa taarifa rasmi ya kufanya hivyo.

Aidha, alisema mabasi 40 ya abiria ya UDA yanatarajia kuanza kazi leo na kutoa ajira kwa watu 8,000.

Alisema mabasi hayo yameongezeka na kufikia 70 na yanatarajia kufanya safari zake katika maeneo mbalimbali yenye shida ya usafiri jijini Dar es Salaam.

Alisema hadi kufikia Juni, 2014, Dar es Salaam itakuwa na mabasi 2,000 na itapunguza adha ya usafiri.

“Simon Group tumeingia ubia na Kampuni ya kutengeneza mabasi Eicher na Africariers na lengo ni kuboresha huduma ya usafiri katika viunga vya Dar es Salaam,” alisema Kisena.

Aliongeza kuwa katika mipango hiyo yatakuwapo mabasi ya wanawake na watoto yatakayozingatia makundi ya watu wenye mahitaji maalumu.

Hivi karibuni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, alisema uamuzi wa kujitoa uliamriwa na kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwa ajili ya kujadili mwenendo wa shirika hilo.

Alisema tangu UDA ianzishwe mwaka 1974 imekuwa ikijiendesha kwa hasara na kuwa na madeni makubwa.

Alisema maagizo na maazimio ya kujitoa katika umiliki wa hisa katika UDA ni kuachana na maombi ya mwekezaji huyo ya kutaka kununua asilimia 49 ya hisa za Serikali.

Alisema mwekezaji Simon Group anatakiwa kulipa hisa zilizogawiwa kwa bei ya soko la Sh 1,618 badala ya Sh 145.

Alisema hisa za Jiji zikiuzwa kwa bei ya soko la sasa zinakadiriwa kuzalisha Sh bilioni 11 hadi 18.

“Fedha hizo zikipatikana zitaingia katika miradi mbalimbali, mfano mradi wa machinjio,” alisema Dk. Masaburi.

No comments:

Post a Comment