Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa klabu
za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea
timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex
Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine
Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam)
ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30)
pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo
kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano
(kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa
awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha
kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza
hadi atakapolipa fedha hizo.
Vilevile Kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa
kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya wachezaji
na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi
Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, Kamati imeagiza
wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho
wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini
(work permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa (Agosti 23 mwaka huu) ili
kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi
hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo
hazikuafikiana.
No comments:
Post a Comment