aaaaa

Pages

Ads 468x60px

Wednesday, November 27, 2013

Naibu Waziri wa Nishati atakiwa kuwaomba RADHI wananchi baada ya kuwaambia kuwa atakayeshindwa kumudu gharama mpya za umeme atumie kibatari



KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemtaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kutoa kauli ya kukatisha tamaa.
 
Simbachawene,  juzi alitoa kauli ya serikali ya kupandisha bei ya umeme kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lilivyoomba hivi karibuni kutaka kuongeza gharama za nishati hiyo kwa asilimia 68.
 
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa hata TANESCO ikiongeza gharama za umeme hadi kufikia sh 800 kwa uniti bado bei hiyo itaendelea kuwa nafuu ukilinganisha na  gharama za kununua mafuta ya taa.
 
Simbachawene alitoa tahadhari kwamba endapo kuna mwananchi yeyote atakayeona gharama za umeme ni kubwa ni vema akaamua kuwasha kibatari au akae gizani.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema kuwa kauli hiyo inaweza kusababisha vurugu kutokana na suala la umeme kumgusa kila Mtanzania.
 
Alisema kuwa hivi sasa viongozi wamekuwa wakitoa kauli za kuudhi ambazo ni hatari kwa ustawi wa taifa.
 
“Tunakumbuka kauli za kuudhi zinavyozidi kushamiri wakti ule aliyekuwa Waziri wa Fedha Basili Mramba alipowaambia Watanzania wajifunge mikanda kubana matumizi hata ikibidi kula majani watakula, lakini ndege ya rais lazima inunuliwe; akaja Waziri wa Ujenzi John Magufuli aliyewaambia wakazi wa Kigamboni kuwa kama hawawezi kulipa ongezeko la nauli mpya basi wajifunze kupiga mbizi, ili kuvuka kwa kuogelea, wanaporudi vijijini au wazunguke kupitia Kongowe sasa hii ya vibatari!”alisema.
 
Alisema kuwa ni muhimu viongozi wakahakikisha wanatoa kauli zilizo na hekima ili kuepusha migogoro.
 
Mkurugenzi huyo alisema kuwa baada ya serikali kupandisha gharama hizo, muathirika mkubwa ni mwananchi wa chini.
 
Alisema kuwa wamiliki wa viwanda wanachoangalia ni faida hivyo kupanda kwa bei ya umeme kutasababisha gharama za bidhaa kuzidi kuwa juu zaidi.
 
“Nchi za wenzetu hakuna jambo linaloweza kufanywa bila kushirikisha wananchi lakini hapa kwetu wanaamua tu na mbaya zaidi wanakuja na kauli za kuudhi na kukatisha tamaa kwa kuwa Watanzania ni wapole,” alisema.
 
Dk. Bisimba alisema kuwa ni lazima wafahamu kuwa upole wa Watanzania utafikia kikomo na hiyo inaweza kusababisha hatari kwa taifa.
 
Wiki hii wadau mbalimbali wa umeme likiwamo Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), walipinga maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ya kuongeza gharama za umeme kwa asilimia 67.8.
 
Walisema ongezeko hilo ambalo limelenga zaidi viwanda vikubwa na vya kati litasababisha kupanda kwa bei za bidhaa za viwandani.
 
Mjumbe wa Bodi ya CTI, Samuel Nyantahe, alisema kabla TANESCO haijapandisha gharama hizo ingekusanya madeni yote na kuziba mianya ya wizi wa umeme.
 
Naye Mjumbe wa CCC Thomas Mnunguli, alisema ongezeko hilo ni kubwa na linakosa uhalali hivyo TANESCO ijitathmini na kujipanga upya na ilenge kutoa huduma bora na nafuu.

-Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment