BAADA ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kufunga mjadala wa mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho, agizo hilo limeonekana kufuatwa vema na wajumbe wa Kamati Kuu, lakini limewafungua wajumbe wa Baraza Kuu, Mkutano Mkuu na taasisi za chama hicho.
Tayari imeripotiwa kuwa uamuzi wa chama hicho kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, umeipasua Kamati hiyo katika vipande vya wafuasi wa wagombea uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi ujao, Mwenyekiti wa sasa Taifa, Freeman Mbowe na Zitto.
Miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu wanaotajwa kumwunga mkono Mbowe ni Dk Slaa, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu, Msemaji wa Chama hicho, John Mnyika na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Waliojitokeza waziwazi kumwunga mkono Zitto ni Dk Mkumbo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba ambao kwa hatua hiyo wamevuliwa nyadhifa zao na aliyekuwa Mwanasheria wa Mbowe, Albert Msando ambaye sasa ni Mwanasheria wa akina Zitto.
Wengine wanaotajwa kumwunga mkono Zitto ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti , Said Arfi ambaye uamuzi wa kumvua Zitto madaraka, ulisababisha ajiuzulu nafasi hiyo.
Hata hivyo, Profesa Mwesiga Baregu, ameripotiwa kukionya chama kwa hatua hiyo, akisisitiza kuwa baada ya uamuzi huo wa Kamati Kuu dhidi ya Zitto, chama kilitakiwa kisubiri baraka za Baraza Kuu, ndipo uamuzi huo utangazwe.
Wafuasi Baraza Kuu Jana Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Temeke na mjumbe wa Baraza Kuu, Patrick Joseph, alitoa kauli iliyodhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa wanaomwunga mkono Zitto.
Joseph katika kauli yake, alionekana kuungana na Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Geita, Abdalah Hamis, ambaye hakumung’unya maneno, kwani aliweka wazi kuwa yeye atamwunga mkono Zitto. Mwenyekiti huyo wa Temeke, aliitisha mkutano na waandishi wa habari akimtaka Mbowe, kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza Kuu, ili litoe uamuzi sahihi kuhusu Zitto na wenzake.
Pamoja na kuwa yeye si mjumbe wa Sekretarieti ya chama, inayopanga ajenda za Baraza Kuu, Joseph alisema ajenda ya kikao cha Baraza hilo, ni kutaka viongozi wawaeleze wajumbe kwa nini wamesambaza waraka wanaodhani unawadhalilisha Zitto, Dk Mkumbo na Mwigamba, wakati waraka huo umekidhalilisha chama kwa kuonesha udhaifu wa Mwenyekiti na Katibu Mkuu.
Akionekana kuwasemea wajumbe wenzake wa Baraza hilo, Joseph alisema katika mkutano huo, wajumbe watataka waelezwe kwa nini wasiamini kwamba uamuzi huo umeathiriwa na hofu ya uchaguzi wa ndani wa chama.
Pia watataka sababu zilizoifanya Sekretarieti ya Kamati Kuu, itangaze ratiba ya uchaguzi mkuu wa ndani, baada ya kuwachafua miongoni mwa watu waliotarajiwa kugombea nafasi, mpaka kuwavua uanachama.
Mjumbe huyo bila kuonesha hofu ya kuvuliwa madaraka kama wenzake walivyofanyiwa, alisema umefika wakati wa kuijenga Chadema bila kufuata masuala ya ubaguzi wa kidini, kikabila ama kikanda kama ambavyo inajulikana nje.
Akifafanua hoja hiyo ya ubaguzi, alisema kuwapo kwa Zitto na Arfi katika nafasi za viongozi wa kitaifa, ilikuwa ni ishara ya kutokuwa na udini ndani ya chama.
"Sasa inawezaje kuwatimua na kuwaita wasaliti watu ambao mmekuwa mkijivunia kuwa ni ishara kwamba hakuna udini?"
Alihoji Mwenyekiti huyo wa Chadema Temeke, na kusisitiza kuwa hayuko tayari kuburuzwa wala kuruhusu baadhi ya viongozi waendelee kuibomoa demokrasia wanayoitangaza kila kukicha.
Joseph alisema chama chao kimekuwa na tabia ya kuingia kwenye migogoro kila kinapokaribia kwenye uchaguzi wa ndani hali inayosababisha kuchafuana na kutukanana miongoni mwa viongozi kwa kuitana wahaini na wasaliti.
Alisema amefadhaishwa na uamuzi wa Kamati Kuu dhidi ya Zitto na Dk Mkumbo, kwani haikuwa na mamlaka ya kikanuni wala kikatiba kufanya hivyo na kuutangaza kwa umma.
Kauli hiyo ya Joseph, ilitolewa pia na Dk Mkumbo, Msando ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu na Profesa Baregu. Hata hivyo, imekuwa ikipingwa na Lissu kwa kutumia Katiba hiyo hiyo ya Chadema, kwamba kuna kipengele kiliongezwa katika Katiba ya sasa, kinachoruhusu Kamati Kuu kuchukua uamuzi kama huo inapoona inafaa.
Joseph alisisitiza kuwa haingii akilini chama kinachopanga mikakati ya kushika Dola, kifukuze na kuogopa watu wanaopanga mikakati ya wao kushinda uchaguzi ndani ya chama.
"Kama ni kweli kupanga mikakati ya uchaguzi ndani ya chama ni uhaini na usaliti, basi operesheni zetu za chama ikiwemo ya M4C zenyewe zinapaswa kuwa uhaini uliopitiliza kwa kuwa nayo ni mikakati ya chama kushika Dola," alisema Patrick. Mikoani Juzi Katibu wa Mkoa wa Geita, Hamis alitamka:
“Nikiwa Katibu wa Chadema, Mkoa wa Geita nasema mimi na wenzangu pia wote ndani ya mkoa wetu tutakuwa nyuma ya Zitto. Nyakati za uonevu, manung'uniko na kubaguliwa sababu tu za eneo, ukanda, udini na kuchaguliana marafiki zimekwisha.”
Katibu wa Chadema wa Wilaya ya Tanga, Harid Rashid, ambaye alifuatana na mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Hussein Baruti na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya ya Tanga, Mohamed Aufi, aliripotiwa kusema hakubaliani na uamuzi wa Kamati Kuu.
Rashid alisema Kamati Kuu ilikuwa na njia nyingi za kulipatia ufumbuzi jambo hilo badala ya kuwavua uongozi. Alisema wameamua kuwa wazi kuhusu tukio hilo kutokana na ukweli kuwa Zitto ni mtu muhimu katika uongozi wa chama.
Kundi la vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Zitto jijini Mbeya nao wanadaiwa kurushiana makonde na viongozi wa Chadema katika ofisi ya chama hicho Mbeya Mjini kwa madai ya kutofautiana misimamo kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu. Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Mbeya Mjini, David Mwambigija ‘Mzee wa Upako’, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo juzi mchana.
Mjadala wafungwa Kudhihirisha kuwa wajumbe wa Kamati Kuu wametii agizo la Dk Slaa la kufunga mjadala huo, jana gazeti hili lilipotafuta namna ya kumpata Mwigamba, alikuwa akikata simu zake.
Lilipomtafuta Profesa Baregu, alipokea lakini alijibu kwa ufupi kwamba kwa sasa hawezi kuzungumzia mambo ya Chadema. Wafuasi wa Mbowe Baada ya Zitto na Dk Mkumbo kuzungumza baada kuvuliwa madaraka, Mnyika na Lissu waliitisha mkutano na waandishi wa habari kukanusha yote yaliyozungumzwa.
Katika mkutano wao akina Mnyika, walidai kuwa waraka uliochapishwa na magazeti kuwa ndio uliomponza Zitto kwa kuwa si uliowasilishwa mbele ya Kamati Kuu.
Lakini mwandishi wa waraka huo, Mwigamba alijibu haraka kuwa hakuna kilichohaririwa bali waraka huo ndio sahihi. Kutokana na vurugu zilizotokea Kigoma, wafuasi wa Mbowe walisema ni za kutengeneza na leo wamejipanga kufanya mkutano kutetea hoja kuwa Kigoma anakotoka Zitto, wanaunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu.
Mbali na kikao hicho cha Kigoma, pia Mratibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Chasso), Dar es Salaam, Elihuruma Himida, alisema leo umoja huo utatoa kauli kupinga matamko ya wanaojiita wanafunzi wa vyuo vikuu, waliosema watazunguka nchi nzima kumwunga mkono Zitto.
Elihuruma pia alidai kuwa mkutano wa Zitto kujibu hoja za kuvuliwa madaraka, uliandaliwa na wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), akina Juliana Shonza, waliohudhuria mkutano huo wa Zitto, huku viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), wakizuiwa kumsikiliza kiongozi huyo.
----Habari Leo
No comments:
Post a Comment