UKATILI! Katika hali ya kusikitisha, mtoto mwenye umri wa miaka 8 aliyejitambulisha kwa jina la Loveness na mwenzake aitwaye Anna, wanadaiwa kulazimishwa kufanya kazi za ndani huku wakipata vipigo vikali kutoka kwa waajiri wao.
Loveness alikuwa akifanyishwa kazi Ubungo-Maziwa na Anna alikuwa Kimara jijini Dar.
Watoto hao wameeleza kazi nzito wanazofanyishwa katika mazingira magumu wakiwa na umri mdogo, wanaohitaji kwenda shule.
“Mama (mwajiri wake) alikuwa akinipiga na wakati mwingine kunichanja na kisu,” alisema Loveness.
Majirani ambao hawakupendezwa na matukio hayo, waliitonya Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers ili kufuatilia suala hilo.
Jirani mmoja ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alidai kwamba alikuwa akiumizwa na mwajiri wa Anna ambaye alikuwa akimpa vipigo vikali mtoto huyo ambaye alikuwa akimlea mtoto wa mama huyo kila siku.
“Hakuna kitu kilichokuwa kikituumiza majirani kama mtoto Anna ambaye alikuwa akipata vipigo vikali kila siku iendayo kwa Mungu kutoka kwa mwajiri wake, heri arudi kwao,” alisema.
Mtangazaji wa kipindi cha Wanawake Live kinachotetea haki za watoto na wanawake kupitia EATV, Joyce Kiria alitinga nyumbani kwa waajiri hao na kumkamata mmoja wao kisha kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Kimara, Dar kwa ajili ya kujibu mashitaka ya kukaa na mtoto mdogo kama mfanyakazi.
Hata hivyo, mtangazaji huyo aliamua kuwachukua watoto hao na kwenda kuishi nao nyumbani kwake Changanyikeni, Dar, kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kuwasafirisha vijijini kwao ambapo Loveness anatokea Morogoro na Anna ametokea Singida.
Joyce amekuwa akifanya mawasiliano na familia za watoto hao ili kuwarejesha kwao huku Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Sophia Simba na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka wakiombwa kuangalia suala hilo la unyanyasaji kwa watoto kwa umakini mkubwa.
No comments:
Post a Comment