MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amesimulia namna alivyovamiwa na kupigwa na Wanachadema wenzake mithili ya mwizi.
Mwigamba alipata kipigo hicho mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya uongozi wa juu wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei katika ukumbi wa Hoteli ya Coridal Spring, jijini Arusha wakati wa Mkutano wa Baraza la Uongozi la Chadema, Kanda ya Kaskazini.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Mwigamba ambaye ameahidi kuweka kila kitu wazi leo, alisema yeye hakupigana bali alipigwa na anamtuhumu kiongozi wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), aliyemtaja kwa jina la Noel Olewaroya, kuwa ndiye aliyeanza kumpiga.
Kiongozi huyo anayesubiri barua ya kusimamishwa uongozi, baada ya kupata taarifa za hatua hiyo katika vyombo vya habari, alidai kuwa kijana huyo na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ndio walioanza kumshambulia wakilenga kumnyang’anya simu na kompyuta yake ya mkononi ndani ya mkutano huo.
Kwa mujibu wa madai ya Mwigamba, Lema alikuwa akisema nataka simu na yeye akamjibu kuwa hatampa na wakati akienda kumnyang’anya, kuna mmoja wa wajumbe aliwahi kumshika Mbunge huyo.
“Wakati Lema ameshikiliwa, huyu Noel ambaye hakuwa mjumbe wa kikao nadhani ni mtandao wa Lema, alitokea huko akanikwida akanipiga ngumi ndio na mimi nikalazimika kujibu.
“Nilitoa simu kwa Katibu wa Kanda, Aman Golugwa, na hali ikawa imetulia lakini kumbe Lema alikwenda nje kuchukua jiwe linalotumika kupanga barabarani akanirushia kichwani…nilikwepa na kwa bahati mbaya nikaanguka nikapiga kichwa nikaota nundu…si kubwa sana,” alisimulia Mwigamba.
Baada ya hapo, kikundi cha vijana wa Chadema maarufu Red Brigades, kwa mujibu wa Mwigamba, kilimvamia na kumbeba na kumtoa nje ya ukumbi kama mwizi huku wakimpiga mateke.
“Unafahamu Tanganyika Jeki? Ndivyo walivyonibeba huku wakinipiga mateke mpaka nje…wakati huo Mbowe alishatoka nje na ninadhani kompyuta yangu na simu walikuwa wakipeleka kwake,” alidai.
Alidai alipofikishwa nje, alimuona Mbowe akiwa katika gari lake amefunga vioo na vijana hao walimbeba kwa mtindo huo wa Tanganyika Jeki mpaka mbele ya gari hilo, wakamsimamisha kisha wakampiga mtama akadondoka chini.
“Nilimwambia Mbowe aliyekuwa akishuhudia kuwa anachofanya si vizuri, lakini hakujibu mpaka Katibu wa Kanda, Golugwa, alipokuja wakanitoa na kuniweka pembeni,” alisema. Muda mfupi baada ya hapo, alisema gari la Polisi lilifika ndipo akaingizwa ndani yake na kupelekwa Polisi.
Gazeti hili lilimtafuta Mbowe kuhusu madai ya Mwigamba kupigwa mtama mbele ya gari lake huku akishuhudia, lakini akalalamika kwamba yeye si gari na kutaka aelezwe wapi gazeti hili, lilipata taarifa kwamba yeye amempiga ngumi Mwigamba.
Mwandishi alipomtaka asome vizuri gazeti la HabariLeo Jumapili, kwamba halijaandika taarifa za yeye kumpiga ngumi Mwigamba, alijibu kwamba suala hilo, kuna wasemaji wa chama, ndio wanaopaswa kulizungumzia.
Lema anayetuhumiwa na Mwigamba kuanzisha vurugu hizo, kumrushia jiwe, kuagiza vijana kumpiga, alipopigiwa simu, iliita bila majibu. Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Chadema, John Mnyika, kuhusu pamoja na mambo mengine, hatua ambazo chama kitachukua dhidi ya kiongozi wa Bavicha, Noel anayedaiwa kumpiga Mwigamba ngumi na kuingia katika kikao ambacho hakuwa mjumbe, lakini simu yake iliita bila majibu kama ya Lema.
Baadaye Mnyika alipiga simu na kuagiza Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, atafutwe kwa kuwa alikuwa eneo la tukio, na alipotafutwa alipatikana kuomba muda apige mwenyewe.
Golugwa akizungumzia hali ilivyokuwa, alidai Mwigamba alitoa mada kuhusu hali ya uhai wa chama katika mkoa wake ambapo aliwapongeza viongozi wakuu wa chama hicho.
“Lakini tunashangaa tukiwa bado hatujamaliza kikao, Mwigamba alituma taarifa za uzushi katika mtandao wa Jamii Forum na kwa kutumia wataalamu wa Chadema wa teknohama, walifuatilia nani aliyetuma wakafanikiwa kumbaini kuwa aliyefanya hivyo ni Mwigamba,” alidai.
Mwigamba pamoja na mambo mengine, anadaiwa kutoa taarifa katika mtandao huo kuwashutumu Mwenyekiti wa Taifa na maofisa wengine wa chama, kwamba wanatumia fedha nyingi kuzunguka na kufanya vitu ambavyo havieleweki.
Alidai baada ya kuelezwa alichokifanya, awali Mwigamba alibisha kwa kutoa maneno ya vitisho kwa Lema kwa maneno ya uchonganishi.
“Tulimwonea huruma tu Mwigamba alikuwa mtu mwenye sifa nzuri ndani ya chama na alikuwa anapambana haswa, lakini hatuwezi kubeba mizoga, amedanganywa na watu ambao hawaitakii mema nchi,” alidai.
No comments:
Post a Comment