Kikosi cha mgambo
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeanza utekelezaji wa kudhibiti uchafu katika maeneo yake yote, kwa kutoa mafunzo kwa vikundi 58 vya ulinzi shirikishi vya usafi wa mazingira ili kusimamia zoezi hilo.
Akifunga mafunzo hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Meya wa Kinondoni, Diwani wa Kata ya Kigogo, Richard Chengula, alisema lengo la mafunzo hayo ni kutoa weledi na mbinu za kazi katika kuwakamata wahalifu watakaotupa taka ovyo.
Alisema sheria itafuatwa katika kuwakamata wahalifu na kwa kila kosa mtuhumiwa atotozwa faini ya Sh. 50,000 na kupatiwa risiti.
“Zoezi linaanza wiki ijayo (leo), ili kufanikisha Manispaa kuwa safi, kila mwananchi anatakiwa kuuchukia uchafu,” alisema Chengula.
Chengula alisema, Manispaa hiyo huzalisha tani 2,026 za taka kwa siku na ina uwezo wa kutupa taka tani 1,560 ambazo ni sawa na asilimia 76, asilimia 23 ambazo ni sawa na tani 466 za taka hizo huzagaa mtaani.
“Hivyo mafunzo haya ni mkakati wa mabadiliko ya kuimarisha shughuli za usafi wa kuleta mabadiliko endelevu kwa wananchi kwa kuelewa sheria, kanuni na taratibu za afya na mazingira,” alisema.
Mafunzo hayo yalitolewa siku mbili kwa washiriki 178 kutoka vikundi vya ulinzi shirikishi vya usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo, kauli mbiu ni ‘Kinondoni uchafu sasa basi.’
No comments:
Post a Comment