Mkuu wa mkoa wa mwanza Evarist Ndikilo
Watu wawili mmoja akiwa na silaha ya kivita wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia na kuweka chini ya ulinzi ofisi ya mauzo ya tiketi ya kivuko cha Busisi akiwamo ofisa wake na kisha kupora kiasi cha fedha ambacho bado hakijafahamika.
Tukio hilo lilitokea saa 3:15 usiku wa kuamkia jana baada ya watu hao mmoja akiwa na panga na mwingine bunduki aina ya SMG huku akifyatua risasi kadhaa hewani kuwatisha wananchi. Watu hao wanadaiwa kumlazimisha ofisa aliyekuwa anauza tiketi awapatie fedha zote.
Katika tukio hilo ambalo lilidumu kwa takribani dakika 10, mtu mmoja aliyekuwa anakata tiketi alijeruhiwa mguuni baada ya kukaidi amri ya kujisalimisha.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Busisi, Tumani Thomas, alisema hali hiyo ilisabaisha wakazi wa eneo hilo hususani wafanyabiashara walipata hofu kutokana na milio ya risasi.
“Bado kuna utata katika tukio hilo nadhani lengo lao kubwa lilikuwa ni kuvamia feri hizo na kuwapora abiria, kwa bahati zilikuwa ziwani huenda kuna kitu kilichotibua mpango wao huo…majeruhi alikimbizwa Hospiatli teule ya Wilaya ya Sengerema usiku huo na polisi walifika ndani ya muda mfupi,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi, Ernest Mangu, amethibitisha tukio hilo na kusema kwamba alikuwa na taarifa za awali hivyo atatoa ufafanuzi zaidi leo. Tukio hilo limekuja siku mbili toka Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo na Kamanda Mangu kusisitiza kuwa kulikuwa kunaandaliwa mkakati kabambe wa kuimarisha ulinzi na usalama mkoani humo kupitia falsafa ya ulinzi shirikishi.
No comments:
Post a Comment