Mama wa MwanaHip Hop aliyewahi kuaminika kuwa bingwa wa mitindo huru, Albert Mangwea aliyefariki mwezi Mei mwaka huu, Denisia Costantine Mangwea ameibuka na kumtetea mwanamuziki wa kizazi kipya Hamis Mwin’juma ambaye anatuhumiwa kuahidi pesa kwa mama huyo na kuingia mitini.
Sakata hilo ambalo limekuwa likiripotiwa tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, linatokana na kitendo cha mwanamuziki huyo (MwanaFA) ambaye aliwahi kuahirisha onesho lake, baada ya kifo cha msanii mwenzake (Albert Mangwea), kutokuweka hadharani hitimisho la ahadi aliyoitoa kwa familia ya marehemu.
Tarehe 31 ya mwaka huu ilikuwa ni tarehe ya onesho la The Finest ambalo MwanaFA alikuwa akitimiza miaka 13 ya muziki wake, akawa na lengo pia na kuugeuza muziki wa Hip Hop uwe na sura ya kistaarabu na kibiashara pia ili kuuongezea aina ya mashabiki.
Siku moja kabla ya onesho, msiba wa Albert Mangwea ukatokea, na hapo ikamlazimu mwanamuziki huyo kuahirisha onesho lake, na kulisogeza wiki mbili mbele huku akiahidi asilimia 15 ya faida atakayopata, angeipeleka kwa familia ya Albert Mangwea.
Baada ya mazishi, Onesho la The Finest lilifanyika Juni 14, na baada ya hapo, MwanaFA hakuonekana akisema kwenye mitandao wala kwenye redio kuhusiana na mapato yake kwenye onesho hilo na kiasi gani alipeleka kwa Mama Mangwea. Tangu onesho hilo, huu ni mwezi wa tatu na ndipo gazeti moja la kila wiki likaandika kuhusiana na suala hilo, jambo ambalo linaendelea kuzungumzwa kila kukicha kwenye vyombo vya habari. Na ndipo gazeti hili liliamua kwanza kumtafuta Mwana FA na kuongea naye.
Kauli ya MwanaFA
Akiongea na Mwananchi, MwanaFA alikiri kuahidi kutoa fedha hizo na aliahidi asilimia 15 ya faida itakayotokana na mapato ya onesho la The Finest.
“Nakiri kukosea jambo moja, nilipoahidi, niliongea na wanahabari lakini wakati wa kutoa, nilitoa bila kutangaza, na hii kutoa jamani ni moyo, haina haja kumtangaza mtu kwa kuwa umemsaidia au umempa pole”, alifafanua MwanaFA
Alisema katika mapato aliyoyapata kutokana na onesho hilo ambayo yalikuwa ni jumla ya shilingi 19.5 milioni, alitoa milioni tatu na kuzikabidhi kwa mama huyo, ingawa si taslimu, aliziingiza kwenye akaunti yake, katika benki ya Exim. Alifafanua kwamba alilifanya hili kwa moyo na hakuwa na nia ya kujitangaza kwa hiyo alilimaliza akawa anaendelea na shughuli zake. Baada ya kauli hii, Mwananchi likapiga mguu mpaka Kihonda kwa mama yake Mangwea, Bi Denisia Costantine Mangwea
Mama Mangwea ashangaa!
Alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo Mama Mangwea alikiri kwamba ameumia sana moyo baada ya kusikia ripoti ya kwamba MwanaFA anadaiwa hakutoa hizo pesa kwani alitoa kipindi kile kile cha msiba.
“Kabla hata ya arobaini, aliweka benki kisha akaja na mwenyewe, hakuna na waandishi kama wanavyofanya wenzake, alikuja mwenyewe tukaongea, na mara kwa mara tunawasiliana, wanataka kumtia doa kijana wa watu ni muungwana sana”, alifafanua mama Mangwea.
No comments:
Post a Comment