MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Joseph Kaniki amepandishwa kizimbani jijini Addis Ababa, Ethiopia kutokana na tuhuma za kukamatwa na madawa ya kulevya.
Iwapo Kaniki pamoja na mwenzake Mkwanda Matumla ambaye ni bondia watapatikana na hatia, basi watafungwa nchini Ethiopia hadi watakapomaliza kifungo chao, Serikali ya Tanzania imethibitisha hilo.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo ameliambia Championi Ijumaa, jana kutoka Addis Ababa kuwa, Kaniki na Mkwanda walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa wiki na huenda ikawa hivyo tena wiki ijayo.
“Jana (juzi) tulikwenda kuwaona na tumekuwa tukifuatilia kwa karibu, huku kidogo kuna utaratibu tofauti, hivyo hatujajua lini watapandishwa tena kizimbani kwa mara ya pili.
“Iwapo watapatikana na hatia, kama ni kifungo cha jela, basi watatumikia hapa Ethiopia. Maana tunabanwa kutokana na kutokuwa na mkataba wa kupeana washitakiwa au wafungwa kama ambavyo nilieleza awali,” alisema Shelukindo.
“Hii juzi tu, kuna Watanzania wengine walikuwa wamefungwa hapa na tayari wameshamaliza vifungo vyao, wameondoka kurejea nyumbani.
“Lakini tumekuwa tukifuatilia kwa karibu, lengo ni kuhakikisha hata kama watuhumiwa au wakihukumiwa, basi haki yao inapatikana. Uingereza, Marekani na nchi nyingine wamekuwa wakifanya hivyo.”
Lakini taarifa nyingine ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa Mtanzania anayeishi Addis Ababa, zinaeleza Kaniki amekuwa akilia gerezani usiku kucha.
“Kuna Watanzania wenzetu wamefungwa katika gereza ambalo Kaniki yumo, tulienda kuwaona juzi, yeye hatukumuona. Ila wanasema amekuwa akilia usiku kucha, tena wakati mwingine kwa sauti ya juu akionekana kulijutia suala hilo,” alisema Mtanzania huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Kaniki na Mkwanda walikamatwa siku kadhaa zilizopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Addis Ababa nchini humo wakiwa njiani kwenda barani Ulaya na taarifa zinaeleza wangetua Italia, nyingine Hispania lakini wawili hao wanaishi Sweden.
Kaniki amewahi kuzichezea Simba, Mtibwa Sugar na Rayon Sports ya Rwanda, alikwenda kufanya majaribio Sweden ambako alifeli lakini baadaye akasajiliwa na timu ya daraja la pili ya Konya ambayo hata hivyo, hakudumu nayo na kazi yake ya mwisho ilikuwa ni ufagizi katika kampuni ya usajili mjini Norrkoping.
No comments:
Post a Comment